1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya nguruwe yabadili sura

1 Mei 2009

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limeongeza makali ya tahadhari ya kusambaa kwa homa ya nguruwe hadi awamu ya tano .Kauli hiyo inaashiriia kuwa sasa wanadamu wanaweza kuambukizana homa hiyo iliyozuka Mexico

https://p.dw.com/p/HguV
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO,Margaret ChanPicha: AP

Kadhalika homa hiyo inaweza kusambaa kutoka taifa moja hadi jengine, mawili kwa uchache.Mambukizi mapya yameripotiwa zaidi barani Ulaya katika mataifa ya Ujerumani,Austria na Uswisi.Mexico kwa upande wake imeamuru afisi zote za serikali zisizotoa huduma za dharura kufungwa kuanzia hapo kesho ili kupunguza uwezekano wa kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.


Shirika la Afya Ulimwenguni limeongeza makali ya tahadhari hiyo baada ya visa vya maambukizi kuripotiwa kutokea katika mazingira ambayo hayakuhusiana na nguruwe au kukutana na wagonjwa waliozuru Mexico.Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO Margaret Chan alitoa wito wa tahadhari zote kuchukuliwa ili kupambana na hali iliyopo sasa,''Mataifa yote yanapaswa bila kupoteza muda wowote kujiandaa na mipango yao kupambana na janga.Sharti kila nchi iwe chonjo kuchunguza visa vya maambukizi ya homa ya aina yoyote vilevile pneumonia.''



Keiji Fukuda, WHO
Keiji Fukuda Mratibu wa mpango wa kupambana na Influenza, WHOPicha: AP

Tahadhari hizo zimetolewa baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa kwa sasa maambukizi mapya yaliyoripotiwa hayakutokea kwenye nguruwe au baada ya kutangamana na watu walioizuru Mexico hivi karibuni.Mratibu wa mpango wa kupambana na Influenza katika Shirika la Afya Ulimwenguni WHO amesisitizia umuhimu wa maabara za kila nchi kuimarisha uwezo wao wa kuwapima watu wanaoshukiwa kuambukizwa virusi hivyo vilevile kuwa chonjo,''Virusi hivi vilitokea kwenye nguruwe mara ya kwanza lakini kwa sasa vinaonekana vikiwa kama vile vinavyosababisha mafua katika binadamu yanayoambukiza.Kwa sasa hakuna ushahidi kuwa watu wanaambukizwa na nguruwe,hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kula nyama au bidhaa za nguruwe kunaleta madhara yoyote.Inaonekana kuwa virusi hivi vinasambaa kati ya wanadamu kwa sasa'' alifafanua.


Vifo vilivyosababishwa na virusi hivyo vimeripotiwa kutokea Mexico na Marekani pekee kwa sasa.Maambukizi mengine yameripotiwa kutokea Mexico kwenyewe,Marekani,Canada,Uingereza,Israel,New Zealand,Ujerumani,Austria na Uhispania.

Kufuatia hali hiyo Rais wa Mexico Felipe Calderon ameamuru kufungwa kuanzia kesho Mei mosi kwa kipindi cha siku tano kwa afisi za serikali zisizotoa huduma za dharura.Wakazi wa nchi hiyo kadhalika wameagizwa kubakia majumbani mwao wakati ambapo juhudi za kupambana na virusi hivyo zinaendelea,.



Schweinegrippe Mexico
Wakazi wa Mexico wamelazimika kuvaa vichuja puaPicha: AP

Tayari maduka mengi na shule zimefungwa tangu baa hilo kuzuka mwanzoni mwa wiki hii.Hatua hiyo inaripotiwa kuuathiri uchumi wa Mexico hasa baada ya mataifa mengine ya kigeni kuwaonya raia wao kutoizuru bila ya sababu za msingi.Kabla ya janga hilo kutokea uchumi wa Mexico uliripotiwa kunywea kwa asili mia 8 katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita.


Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limeonya kuwa ulimwenguni huenda ukakabiliwa na janga kubwa hasa baada ya mtoto mmoja kufariki huko Marekani baada ya kuingia jimbo la Texas kutokea eneo linalopakana na Mexico.Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Margaret Chan amesisitiza kuwa hii ni fursa ya kuonyesha mshikamano kote ulimwenguni na alisema''Hii ni fursa ya kuonyesha mshikamano kote ulimwenguni wakati ambapo tunajitahidi kutafuta suluhu na njia zitakazozinufaisha nchi zote.Wanadamu ndio walio hatarini zaidi kunapozuka baa lolote lile.Kama nilivyosema hatuna suluhu ila tutayapata majibu yote.''


Umoja wa Ulaya kwa upande wake umeeleza kuwa uko tayari kupambana na janga lolote lile.Shirika linalohusika na uzuwiaji na udhibiti wa magonjwa la Umoja huo limesema kuwa liemkuwa likishirikiana na nchi wanachama tangu mwaka 2005 kuunda mbinu madhubuti za kupambana na majanga.Shirika hilo limefafanua mbinu itakazotumia zikiwemo uangalizi wa kina,vipimo,tiba mujarab pamoja na matumizi ya dawa za kupambana na virusi hivyo za Tamiflu na Relenza.Mawaziri wa Afya wa Umoja wa Ulaya wanakutana Luxembourg kwa dharura hii leo.



Wakati huohuo serikali ya Misri iliamuru kuchinjwa nguruwe laki nne alfu nchini humo kama njia moja ya kuepuka maambukizi.Hata hivyo Umoja wa Mataifa umekosoa hatua hiyo.Ifahamike kuwa Misri imekuwa ikitatizwa na homa ya ndege iliyosababisha vifo vya watu 26 mpaka sasa.Wataalam wa afya wanahofia kuwa kuzuka kwa aina nyengine ya homa huenda kukasababisha hasara kubwa nchini humo.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya /RTRE,AFP,DPAE

Mhariri:Oumilkheir Hamidou