1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Horst Köhler-kipenzi cha bara la Afrika

Oumilkher Hamidou1 Juni 2010

Jinsi Horst Köhler alivyokua akitoa kipa umbele kwa masuala ya Afrika alipokua rais wa shirikisho-hakuna mwanasiasa yeyote anaeweza kumpita upande huo

https://p.dw.com/p/NeZv
Horst Köhler akitangaza kujiuzu kwakePicha: AP

Mataifa 12 ya Afrika aliyatembelea Horst Köhler alipokua rais wa shirikisho.Hakuna mwanasiasa yeyote mwengine aliyelipigania zaidi bara hilo jirani,kumpita yeye.Ute Schaeffer,mkuu wa matangazo kwaajili ya Afrika na Mashariki ya kati,ya Deutsche Welle alifuatana nae katika ziara zote hizo barani Afrika.

Sikufikiri kama hii ingekua mara yake ya mwisho kujitokeza rasmi hadharani.Katika hafla ya fasihi iliyofanyika saa za asubuhi,Horst Köhler alikua achambue kitabu chake alichokipa jina "Schiksal Afrika" au Mustakbal wa Afrika na mie ndie niliyekua niongoze majadiliano pamoja na rais wa shirikisho.Kila kitu kiliandaliwa ipasavyo katika kasri la Schloss Bellevue.Watu wote wanaovutiwa na siasa ya Köhler kuelekea Afrika walifika.Kulikuwepo na wawakilishi wa bunge la shirikisho-Bundestag,wawakilishi wa wakfu,wawakilishi wa ofisi za ubalozi wa nchi za Afrika,waandishi vitabu na wasanii.

Nnachoweza kusema ni kwamba siku ile Horst Köhler alikua kama mwenye mawazo ya mbali.Hajajaribu hata kuanzisha mazungumzo pamoja na wawakilishi wa kutoka Afrika.Hata mzaha hakufanya siku hiyo.Hata bashasha zilikawia kung'ara katika uso wake.Nilijua tangu mwanzo kwanini Köhler hakulijibu vizuri suala kama Afrika itadhibiti pia mhula wake wa pili madarakani.

BdT Köhler unterstützt Dein Tag für Afrika
Horst Köhler katika mojawapo ya kampeni zake kuhusu Afrika,katika kasri la Schloss Bellevue mjini BerlinPicha: picture-alliance/ dpa

Horst Köhler alionyesha amechoka.Mtu hawezi kumlinganisha na mwaka 2004 alipoingia kwa mara ya kwanza madarakani na hapo hapo kufanya ziara yake ya kwanza barani Afrika.

Alianzia ziara yake ya kwanza ya nchi za nje,kule kule ambako baadhi ya wale wanaojiita wanasiasa wanashughulikia masuala ya nchi za nje wanafikiria kuwa ni" mwisho wa dunia."

Kule ambako eti hakuna kinachofanyika:katika nchi masikini kabisa ya dunia-nchini Sierra Leone.

Horst Köhler alikua na kiu cha kujifunza na kujua kipi kinauleta pamoja ulimwengu wa utandawazi-na inakutikana wapi tofauti kati ya maeneo yaliyoendelea na yale yenye maendeleo duni.Aliweza kuweka kando fasaha ya kisiasa na kujisahau kama rais wa shirikisho, masuala ya ubinaadam yanapojitokeza mfano kutahiriwa wakinamama,wahanga wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauwaji ya halaiki.

Hata katika mambo mengine madogo madogo,Horst Köhler alijitokeza zaidi kama binaadam badala ya mwanasiasa.Mfano alipoahidi moja kwa moja kuwapatia wanakijiji mashini ya kuchapisha nakala ,licha ya kujua fika haitapita muda mrefu itaharibika kwa mavumbi.Alikua akihusudu kuona watu wanajitolea na kuwajibika.Miongoni mwao ni wakinamama wa kiafrika wanaochukua mikopo midogo midogo ili kujiendeleza.

Mwandishi.Schaeffer,Ute/Hamidou,Oummilkheir

Mpitiaji:Abdul-Rahman,Mohammed