1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hospitali Kenya 'yawaweka kizuizini' wazazi

28 Desemba 2012

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, hospitali mmoja nchini Kenya inaripotiwa kuwaweka kizuizini wanawake wanaokwenda kujifungua, pale wanaposhindwa kulipia gharama za matibabu na huduma walizopatiwa hospitalini hapo.

https://p.dw.com/p/17AFm
Hospitali nchini Kenya.
Hospitali nchini Kenya.Picha: Reuters

Mkurugenzi wa hospitali hiyo ya Pumwani iliyo karibu na mji mkuu Nairobi, Lazarus Omondi, amesema kwamba hiyo ndio njia pekee ya kuifanya hospitali yake kuendelea kufanya kazi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, tayari kundi moja la haki za binaadamu lenye makao yake makuu jijini New York, Marekani, limefungua kesi mahakamani kuomba kuizuia hospitali hiyo kuendelea na kitendo hicho.

Akinamama wawili wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda karibu na hospitali hiyo ya wazazi wamethibitisha kwamba walikataliwa kuondoka hospitalini baada ya kujifungua, kwani walishindwa kulipa kati ya dola 60 na 160 za Kimarekani, walizokuwa wakidaiwa.

"Walinzi wenye bakora huwapiga akinamama wanaojaribu kutoroka bila kulipa," alisema mmoja wa akinamama hao.

Omondi anasema kwamba suluhisho linalofaa kwa tatizo hilo ni kuwa na programu ya bima ya afya ya kitaifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Josephat Charo