1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya kansela Merkel bungeni mjini Berlin

Oummilkheir1 Machi 2007

Kansela Merkel afafanua sera za umoja wa ulaya kuelekea mkutano wa kilele wiki ijayo

https://p.dw.com/p/CHJ9
Kanasela Angela Merkel
Kanasela Angela MerkelPicha: AP

Kansela Angela Merkel amelihutubia bunge la shirikisho-Bundestag mjini Berlin hii leo,akichambua malengo yanayobidi kutekelezwa na Umoja wa ulaya.Hotuba hiyo imetolewa kabla ya mkutano wa viongozi wa umoja huo wiki ijayo mjini Brussells.Ujerumani ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya.

Akichambua sera za Umoja wa ulaya mbele ya bunge la shirikisho kansela Angela Merkel amezungumzia kile ambacho Umoja wa ulaya unapaswa kukishughulikia ili kujiambatanisha na wakati tulio nao.Kansela Angela Merkel amesema:

“Nnaamini tunaweza kusema,kama ilivyokua mwaka 1957,Umoja wa ulaya unajikuta njia panda.Hii leo muhimu ni kuhakikisha,kilichoshindikana kutekelezwa hadi sasa au kile ambacho hakikutekelzwa kikamilifu,kitekelezwe ili ,kwa upande mmoja ,Umoja wa ulaya uweze kujiambatanisha na majukumu yake mepya na kwa upande wa pili uweze kukabiliana na hali mpya iliyozuka ulimwenguni.”

Katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa ulaya wiki ijayo mjini Brussells Ujerumani inapanga kutoa mapendekezo yake,miongoni mwa mengineyo kuhusu namna ya kuhifadhi ya hali ya hewa .Umoja wa Ulaya unabidi uwatanabahishe walimwengu kwamba usafi wa mazingira na ukuaji wa kiuchumi ni mambo mawili yanayokwenda sambamba.

Hata katika mazungumzo ya shirika la biashara ulimwenguni-duru ya Doha,kansela Angela Merkel anapanga kuzidisha juhudi za Umoja wa Ulaya,ili kuhakikisha yanafanikiwa.

“Kipa umbele kwetu ni kufikia makubaliano katika mazungumzo ya Doha ambayo tutayafuatilizia kwa nguvu.Kwasababu tunajua vyema,sote,Umoja wa ulaya na Ujerumani,bingwa wa dunia katika kusafirisha bidhaa nchi za nje,tutafaidika” ameshadidia kansela Angela Merkel mbele ya wabunge mjini Berlin.

Kansela Angela Merkel ameendelea kusema:

„“Serikali kuu ya Ujerumani , mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya,tunawajibika .Tunataka kuona miradi ya umoja wa ulaya inasonga mbele, lengo likiwa kuwatanabahisha wananchi juu ya umuhimu wa Umoja wa Ulaya na kuiunga mkono miradi yake.“

Upande wa upinzani katika bunge la shirikisho Bundestag mjini Berlin unamkosoa kansela kutopitisha hatua za kijasiri vya kutosha katika kupambana na kuchafuliwa hali ya hewa.

Mada nyengine ambayo bado si bayana ni kuhusu namna serikali kuu inavyopanga kuupatia ufumbuzi mzozo wa katiba ya umoja wa Ulaya-baada ya kukataliwa kwa kura ya maoni ya wananchi wa Ufaransa na Uholanzi.