1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya Obama kwa Arabuni: Visheni ndogo, msaada mkubwa

20 Mei 2011

Hotuba ya Rais Barack Obama inayoakisi sera za nje za Marekani kuelekea Ulimwengu wa Kiarabu baada ya wimbi la mageuzi ya umma kwenye eneo hilo muhimu kwa Marekani haikuonesha dira japo imeahidi msaada kwa mageuzi hayo.

https://p.dw.com/p/11KEF
Rais Barack Obama akitoa hotuba kuhusu ulimwengu wa Kiarabu
Rais Barack Obama akitoa hotuba kuhusu ulimwengu wa KiarabuPicha: AP

Marekani itasaidia mageuzi ya kidemokrasia katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini kwa moyo wake wote. Inapongeza ujasiri wa waandamanaji kwenye mataifa ya Syria na Libya. Inashikilia msimamo wake wa suluhisho la kuwapo mataifa mawili huru ya Israel na Palestina.

Hayo ndiyo mambo makuu ya kushika yaliyokuwamo kwenye hotuba ya Rais Obama, lakini juu ya hapo haikuwa hotuba yenye kuona mbali.

Ukilinganisha na hotuba kama hii kwa Ulimwengu wa Kiislamu aliyoitoa miaka miwili nyuma mjini Cairo, Misri, hotuba hii ya jana haikuwa na ujumbe mpya sana kutoka kwa rais huyo wa Marekani. Kuna machache sana yanayoweza kuitwa ni mageni kutoka kwa Barack Obama.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina
Rais Mahmoud Abbas wa PalestinaPicha: picture alliance/dpa

Moja ni kauli ya wazi ya kutambua kwamba mipaka ya mwaka 1967 ndio msingi wa suluhu ya mgogoro wa Israel na Palestina, kauli ambayo, hata hivyo, tayari imeshapingwa na Israel yenyewe. Lakini hotuba hii pia imeibua ukweli kuwa hata Obama hawezi kuwashambulia hadharani viongozi wa Bahrain na Yemen kwa kuwa ni marafiki wa Marekani.

Cha kufurahisha zaidi ni kile ambacho rais huyu wa Marekani hakukisema kuliko kile ambacho amekisema: Barack Obama amewakumbusha watawala wa Bahrain kwamba majadiliano na wapinzani hayawezi kufanyika ikiwa wapinzani hao wanatupwa gerezani. Lakini hakusema ni kwa namna gani na kwa mkakati gani atamsaidia mshirika huyu wa Marekani kufanya mageuzi ya kidemokrasia yanayohitajika.

Mshirika mkubwa zaidi wa Marekani katika eneo hilo, taifa tajiri la mafuta la Saudi Arabia, hakutajwa kabisa kwenye hotuba hiyo ya Rais Obama, ingawa huko nako upinzani unakandamizwa kwa nguvu zote za kikatili na utawala.

Hili linautia kasoro sana huo unaoitwa mwelekeo wa utawala wa Rais Obama kuelekea wimbi la mageuzi kwenye ulimwengu wa Kiarabu.

Ukweli ni kuwa mwelekeo huo unakumbana na ama kuzivumilia tawala za kidikteta katika eneo hili au kustahmilia hali ya sasa ya machafuko. Hotuba ya Obama sio tu kwamba haizungumzii moja kwa moja mambo hayo, bali pia inaonesha namna alivyojikuta akiwa hana la kufanya mbele ya ukweli huu.

Hatimaye ni kuwa Obama hana dira maalum ya kumuongoza kwenda mbele, maana ukweli ni kuwa Marekani ina ushawishi mdogo sana wa kile kinachoendelea sasa katika Ulimwengu wa Kiarabu.

Lakini, hata hivyo, Obama anaonekana kuchukua hatua: Tunisia na Misri ni vigezo vyema, na ameamua kuzipa msaada mkubwa wa kifedha kuimarisha mchakato wa kidemokrasia zilizouanza. Ni uamuzi mzuri sana ambao hata nchi za Ulaya zinapaswa kuuiga pia.

Mwandishi: Rainer Sollich/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji