1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya Obama yangojewa kwa hamu

P.Martin (AFPE)24 Februari 2009

Rais wa Marekani Barack Obama leo usiku atatoa hotuba yake ya kwanza mbele ya bunge-Congress-kufafanua mpango wake wa kufufua uchumi wa taifa lililokumbwa na wasiwasi kuhusiana na mgogoro wa masoko ya fedha.

https://p.dw.com/p/H0Zd
President Barack Obama listens to second graders at Capital City Public Charter School in Washington, Tuesday, Feb. 3, 2009. (AP Photo/Pablo Martinez Monsiva
Rais wa Marekani Barack Obama.Picha: AP

Ikiwa ni majuma matano tangu kuingia madarakani,Obama atawahutubia Wamarekani moja kwa moja kwa njia ya televisheni.Kawaida hotuba inayotolewa kwenye kikao cha pamoja cha Baraza la Waakilishi na Baraza la Seneti ni mtihani halisi wa kwanza kwa rais alie mpya.Hotuba hiyo humpa nafasi ya kueleza mipango na sera zake za kisiasa.

Lakini Obama tayari amefanikiwa kuungwa mkono na Congress kuhusu mpango wake wa kufufua uchumi ulio na thamani ya dola bilioni mia saba themanini na saba. Vile vile amezindua mpango wa dola bilioni 275 utakaowasaidia wananchi wanaokabiliwa na kitisho cha kunyanganywa nyumba kwa sababu ya mikopo wasioweza kulipa.Lakini hadi sasa jitahada hizo zote hazikuweza kutuliza masoko ya fedha.

Obama ameingia madarakani,wakati Marekani ikikabiliana na msukosuko mkubwa kabisa tangu miaka ya thelathini.Amesema;

"Serikali hii imerithi nakisi ya dola trilioni 1.3 - ni nakisi kubwa kabisa katika historia ya taifa letu."

Baada ya mara kwa mara kuonya juu ya hali mbaya ya uchumi inayokabiliwa nchini Marekani,Obama sasa anataka kuwapa wananchi matumaini kuwa siku za neema zipo njiani-matumaini yaliyochangia kumpatia ushindi katika uchaguzi uliopita.Wasaidizi wake wameeleza waziwazi kuwa licha ya hali mbaya ya uchumi,Obama amepania kuleta mageuzi ya kisiasa yaliyoahidiwa.

Obama ameshasisitiza kuwa masuala yanayohusika na mageuzi katika huduma za afya,ongezeko la joto duniani na jitahada za kukidhi mahitaji ya nishati ni mada zinazohitaji kupewa umuhimu hasa wakati huu ambapo uchumi unadorora.

Katika hotuba yake leo usiku,Obama anatazamiwa pia kutetea mpango wake wa uwekezaji mkubwa katika miradi ya kuzalisha nishati kwa njia mpya zisizochafua mazingira.Kwa maoni yake uwekezaji huo utaanzisha mapinduzi ya kijani yatakayoweza kusaidia ukuaji wa kiuchumi.

Vile vile huenda akajaribu kupunguza tofauti zilizopoo kati ya vyama,licha ya kuwa ni wabunge wachache mno waliounga mkono mpango wake wa kuchangamsha uchumi nchini humo.Mbunge Darrel Issa wa chama cha Republikan alipozungumza na waandishi wa habari katika Ikulu hiyo jana alisema anaingojea kwa hamu kubwa hotuba ya Rais Barack Obama.