1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Rwanda yahujumu haki za binaadamu

15 Agosti 2013

Serikali ya Rwanda inakosolewa kwa kuhujumu uongozi wa Shirika la Kitaifa la Kulinda Haki za Binadaamu – Rwandan League for the Promotion and Defence of Human Rights – LIPRODHOR kwa sababu ya msimamo wake huru

https://p.dw.com/p/19QLm
Human Rights Watch Logo
Human Rights Watch Logo

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limesema watu wanaoaminika kuiunga mkono serikali wamechukua uongozi wa shirika hilo la haki za binadamu la Rwanda katika kile kinachoonekana kuwa mbinu ya serikali kuwabana midomo watetezi wa haki za binaadamu.

Shirika la Haki za Binaadamu la Rwanda LIPRODHOR, ndilo kundi la mwisho lililosalia kuwa na ufanisi nchini humo. Lakini mnamo Julai 21 mwaka huu, idadi ndogo ya wanachama iliandaa mkutano ambao ulipiga kura ya kuichagua bodi mpya. Hatua hiyo ilikiuka sheria za shirika hilo na sheria ya kitaifa kuhusu mashirika yasiyo ya kiserikali.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, wanachama kadhaa wa bodi iliyoondolewa wanafahamika kwa misimamo yao huru na ujasiri wa kukosoa ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa na serikali. Human Rights Watch inasema hatua ya Bodi ya Uongozi Bora ya Rwanda kuidhinisha matokeo ya mkutano huo, bila kuchunguza hoja zilizotolewa na uongozi uliopinduliwa wa kundi hilo, inazusha maswali kuhusu jukumu la shurika hilo la serikali.

Daniel Bekele, ni Mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika. "Badala ya kupinga uamuzi usiofuata sheria wa kuupindua uongozi uliokuwepo na kutetea uhuru na uhalali wa shirika lililosajiliwa kisheria, imefanya kinyume kwa kuutambua uongozi uliochaguliwa kinyume cha sheria na ambao uliondoa uongozi wa awali bila kufuata sheria" Bekele anasema hatua hiyo inapaswa kulaaniwa kwa sababu kama kundi la LIPRODHOR litanyamazishwa, itakuwa pigo kubwa kwa raia wote wa Rwanda.

The Rwandan flag flies in the grounds of the Commonwealth Secretariat at Marlborough House, in London, on March 8, 2010, following a press conference with President of Rwanda Paul Kagame, Trinidad and Tobago Prime Minister Patrick Manning and Commonwealth Secretary-General Kamalesh Sharma. Rwanda was officially accepted in the Commonwealth last year. AFP PHOTO/Carl Court (Photo credit should read Carl Court/AFP/Getty Images)
Serikali ya Rwanda inalaumiwa kukandamiza uhuru wa mashirika yasiyo ya kiserikaliPicha: Carl Court/AFP/Getty Images

Sheikh Saleh Habimana, mkuu wa vyama vya kisiasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kidini katika Bodi ya Uongozi ya Rwanda, anakanusha kuwa shirika lake lina jukumu la kuhakikisha kuwa mashirika yote yanafuata sheria. Anasema bodi iliyopinduliwa ya LIPRODHOR inaweza kwenda mahakamani na kama mahakama itatoa uamuzi kuwa huo ulikuwa uamuzi mbaya basi watabatilisha idhini yao.

Washiriki wa kikao hicho kinachodaiwa kuichagua bodi mpya, waliutaja mkutano huo kuwa wa “mashauriano” na kutathmini uamuzi wa bodi ya LIPRODHOR kujiondoa kutoka Muungano wa Mashirika ya Kulinda Haki za Binaadamu nchini Rwanda - CLADHO.

LIPRODHOR pamoja na mashirika mengine mawili wanachama wa Muungano huo walijiondoa kwa sababu ya migawanyiko ya kindani, ukosefu wa uungaji mkono kutoka mashirika wanachama, na kukosa kuelewana kuhusiana na dosari katika uchaguzi wa bodi ya muungano huo wa CLADHO

Shirika hilo kisha lilikwenda mahakamani kupitia rais wake aliyeondolewa uongozini likitaka kupinga bodi mpya, na kesi hiyo bado iko mahakamani. Jinsi anavyosema Daniel Bekele wa HRW, kama washirika wa Rwanda wanaounga mkono makundi ya kiraia hawataingilia kati kulitetea shirika la LIPRODHOR, hivi karibuni hakutakuwa na mashirika yoyote nchini Rwanda ya kutoa habari huru.

Mwandishi: Bruce Amani/HRW

Mhariri: Iddi Sesanga