1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: wanaharakati wa Congo waachiliwe huru

10 Desemba 2015

Shirika la Human Rights Watch limetaka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo DRC kuadhimisha siku ya kimataifa ya haki za binadamu kwa kuachilia huru walioshiriki shughuli za siasa

https://p.dw.com/p/1HLBF
Joseph Kabila
Picha: AP Photo

Mtafiti mkuu wa maswala ya Afrika Ida Sawyer amesema sharti maafisa nchini Kongo wasitishe mara moja kuogofya na kunyamazisha wanaharakati wanaoandamana kwa amani na wapinzani wa kisiasa.

Amesema siku ya kimataifa ya haki za binadamu ni fursa ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kubadili mtindo wake na kuachilia huru kila mmoja aliekamatwa kwa kujihusisha kwa amani kwenye harakati za kisiasa.

Polisi wafyatua risasi hewani

Katika kisa cha hivi karibuni,tarehe 28 mwezi Novemba katika mji ulio mashariki ya nchi hiyo wa Goma,polisi walifyatua risasi hewani na kutumia hewa ya kutoa machozi wakati karibu watu 100 waliokuwa wakihudhuria maandamano ya amani wakipinga juhudi za serikali kushindwa kusitisha mauaji katika eneo la Beni.Msichana wa umri wa miaka 14 aliuawa na kujeruhiwa.Mamlaka ilikawakamata watu 12,wakiwemo wanaharakati 2 na vijana watatu pamoja na waandamanaji wengine na watu waliokuwa karibu.Vijana hao waliachiliwa huru baada ya siku nne lakini wengine wanaendelea kuzuiliwa kufuatia mashtaka yasiyo ya kweli.

Kwa miaka kadhaa,maafisa wa serikali na wale wa usalama wamewaandama wanaopinga ucheleweshwaji wa uchaguzi wa urais ambao umepangwa kufanyika Novemba mwaka ujao wa 2016 na kuongeza muhula wa utawala kwa Rais Joseph Kabila.

Chini ya katiba ya Kongo,Rais Kabila anatakiwa kuondoka mamlakani Disemba 2016 wakati wa kumalizika muhula wake wa pili.Maandalizi ya uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka ujao hayajaanza.Kabila na wafuasi wake wameonyesha kuwa uchaguzi huenda ukacheleweshwa,huku wakitaja kasoro kwenye orodha ya wapiga kura na gharama ya juu ya uchaguzi.

Polisi na mlinzi wa Republican waliwafyatulia risasi zaidi ya watu arobaini wakati wa maandamano ambayo yalifanyika kwenye mji mkuu Kinshasa na Goma mwezi Janauari ya kupinga mabadiliko yaliyopendekezwa kufanyiwa sheria ya uchaguzi .

Polisi wakimkamata muandamanaji
Polisi wakimkamata muandamanajiPicha: Reuters/Katombe

Maandamano yapigwa marufuku

Mamlaka imeamua kupiga marufuku maandamano ya kisiasa yanayofanyika kwenye miji kote nchini humo huku vijana kadhaa wanaoandamana,wanafunzi,wanamuziki,viongozi wa vyama vya kisiasa na wafuasi wakikamatwa.Shirika la kitaifa la ujasusi ANR waliwazuilia kwa wiki au miezi kadhaa wengi wa waliokuwa wamekamatwa bila mashataka yoyote na bila kuonana na familia zao au mawakili.Wengine wamehukumiwa kwa mashtaka yanayohusiana na siasa.

Kwenye mji ulio kusini mashariki wa Lubumbashi mnamo tarehe mosi Disemba,polisi walitumia gesi ya kutoza machozi kuzuia wafuasi wa timu ya kandanda ya TP Mazembe kuingia kwenye uwanja wa michezo wa kibinafsi kuhudhuria mkutano na kiongozi wa timu hiyo Moise Katumbi ambaye aliwahi kuwa Gavana wa jimbo la Katanga.Katumbi alijiuzulu kutoka chama cha kisiasa cha Rais Kabila mwezi Septemba,akilalamikia ucheleweshwaji wa maandalizi ya uchaguzi.

suala la kuongeza muda wa rais kabila linakabiliwa na upinzani mkali ukiwemo kutoka kanisa Katoliki,mashirika ya kijamii,wanaharakati vijana na waliokuwa wanachama wa muungano wa Rais Kabila ambao wameunda kundi liitwalo G7.Wengi wametaka kuwepo kwa maandamano mapema 2016 ikiwa serikali haitaanza kuandaa mipango iliyo wazi ya kufanyika kwa uchaguzi.

Mwandishi:Bernard Maranga/HRW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman