1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yamkosoa al-Sissi kwa kuruhusu mateso kwa wafungwa

Lilian Mtono
6 Septemba 2017

Ripoti ya shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi ameidhinisha mpango wa mateso magerezani, hatua inayowaruhusu maafisa kufanya maovu bila ya kujali sheria

https://p.dw.com/p/2jQ6i
Ägypten Polizei Polizeiwagen Sicherheitskräfte
Picha: Imago/ZUMA Press

Kwenye ripoti hiyo yenye kurasa 63 iliyotolewa leo hii, shirika la Human Rights Watch limesema al-Sissi, ambaye ni mshirika wa Marekani aliyelakiwa kwa ukarimu kwenye Ikulu ya White House mapema mwaka huu, anajaribu kutafuta utulivu kwa gharama yoyote na ameruhusu mateso kwa wafungwa katika vizuizi mbalimbali ingawa katiba ya Misri inapiga marufuku vitendo vya mateso kwa wafungwa.

Al-Sissi ametoa idhini kwa polisi na maafisa wa usalama kutumia mateso wakati wowote wanapoona inafaa, amesema Naibu mkurugenzi wa masuala ya Mashariki ya Kati kwenye shirika hilo lenye makao yake Jijini New York, Joe Stork. Amesema kuruhusiwa kwa mfumo huo wa mateso kumewaacha raia wakiwa hawana matumaini ya haki.

Kulingana na kundi hilo la utetezi wa haki za binaadamu, madai hayo yanaongeza uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Wafungwa wengi wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu, lililoibuka baada ya uasi wa mwaka 2011 uliomuondoa mamlakani aliyekuwa rais wakati huo Hosni Mubarak, lakini limekuwa likilengwa kwa hatua kali zaidi tangu jeshi lilipompindua rais Mohammed Morsi aliyechaguliwa mwaka 2013.  

Ägypten Präsident Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi anayekabiliwa na shinikizo kutokana na hatua zakePicha: picture-alliance/dpa

Shirika la Human Rights Watch limesema, serikali ya Misri imewakamata na kuwafungulia mashitaka watu 60,000 katika kipindi cha miaka miwili baada ya Mohammed Morsi, ambaye alikuwa mfuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu na baadaye rais wa kwanza wa kuchaguliwa na umma. Mamia ya raia wametoweka katika kile kinachotajwa kama ni utoweshwaji wa kinguvu, na mamia miongoni mwao wanakabiliwa na hukumu ya awali ya kifo.

Kulingana na shirika hilo, mashirika mbalimbali ya utetezi wa haki za binaadamu mara kwa mara ymekuwa yakituhumu idara ya usalama nchini Misri kwa kufanya vitendo hivyo vya utesaji, madai ambayo wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo imeyapinga.

Serikali imekiri kwamba kumekuwepo na visa vya mateso kwa baadhi ya watuhumiwa na polisi wengi wamekuwa wakihojiwa na kufungwa kwa makosa ya vifo vinavyosababishwa na mateso katika miaka ya hivi karibuni.

Shirika hilo limesema liliwahoji wafungwa wa zamani 19 ambao walieleza kwa kina namna mateso hayo yalivyofanyika, ikiwa ni pamoja na kuteswa kwa umeme. Aidha, polisi pia iliwafunga pingu watuhumiwa na kuwaning'iniza kwa kuwafunga mikono yao.

Human Rights Watch Logo Symbolbild
Shrika la HRW linataka Umoja wa Mataifa kuingilia katiPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Ripoti hiyo pia ilimnukuu mmoja wa wafungwa alidai kwamba polisi walimfanyia mara kwa mara vitendo vya ubakaji wakitumia fimbo.

Unyanyasaji unaofanywa na polisi uliongezeka katika kipindi cha maandamano ya umma mwaka 2011 ambayo yaliyomuondoa mamlakani Hosni Mubarak na kuanzisha miaka kadhaa ya mtikisiko mkubwa wa kisiasa.

Sisi, aliyechaguliwa mwaka 2014, aliwataka polisi kuchukuliwa hatua kali kufuatia kuongezeka kwa vifo vilivyosababishhwa na manyanyaso magerezani, pamoja na polisi kuwafyatulia risasi, hatua iliyoibua maandamano na hatimaye baadhi ya polisi kutiwa hatiani kwa makosa hayo.

Kwenye ripoti hiyo, Human Rights Watch imemtaka Sissi kuipa jukumu wizara ya sheria, kwa kuchagua mwendesha mashtaka maalumu atakayeongoza uchunguzi wa madai ya unyanyasaji na kufungua mashitaka.

Iwapo serikali ya Sissi itashindwa kuchukua hatua kali za kukabiliana na janga hilo, tunayataka mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuingilia kati kwa kufanya uchunguzi na kama itawezekana kuwafungulia mashitaka kupitia mahakama za nchini mwao maafisa wa usalama wa Misri na maafisa wengine wanaotuhumiwa kwa kufanya utesaji ama kuruhusu matukio hayo kutokea, kwa kutumia msingi wa kimataifa wa kimahakama, ripoti hiyo imesema.

Mwandishi: Lilian Mtono/afpe,ape.

Mhariri: Iddi Ssessanga