1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda Assad akachukuliwa kama mhalifu wa kivita

MjahidA29 Februari 2012

Marekani imesema rais Bashar al-Assad wa Syria huenda akachukuliwa kama mhalifu wa kivita, huku China ikisema inaunga mkono juhudi za kimataifa za kutuma misaada ya kibinaadamu nchini Syria.

https://p.dw.com/p/14BoU
Rais wa Syria Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa China Yang Jiechi ameyasema hayo baada ya mataifa yenye nguvu ya magharibi kupendekeza azimio la Umoja wa Mataifa la kupeleka misaada ya kibinaadamu nchini Syria.

Akizungumza kwa njia ya simu na mkuu wa Jumuiya ya nchi za kiarabu, Nabil Elaraby, Jiechi amesema jambo la muhimu sasa ni kwa pande zote mbili kujaribu kusitisha mapigano nchini Syria na kuzindua haraka mazungumzo ya kuwa na mabadiliko ya kisiasa.

China ni moja kati ya wanachama watano wa kudumu katika baraza hilo ambayo ina nguvu ya kupinga azimio hilo. China inajaribu kupata hadhi yake ya kidiplomasia baada ya kushutumiwa vikali namna ilivyoshughulikia mzozo wa Syria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary ClintonPicha: dapd

Mataifa ya Magharibi yamesema kwa sasa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaandaa azimio la kurefusha misaada katika maeneo yaliyoathirika nchini Syria huku Ufaransa ikiisihi China na Urusi kutothubutu kupinga azimio hilo kama zilivyofanya katika maazimio mengine ya hapo awali.

Assad kama mhalifu wa kivita

Kwengineko Marekani imesema rais Bashar al-Assad huenda akachukuliwa kama mhalifu wa kivita huku Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya siasa, Lynn Pascoe, akitangaza idadi ya vifo kutokana na mauaji yanayofanywa na vikosi vya serikali ya Assad ikifikia 7,500.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, amesema Rais Bashar Al Assad huenda akachukuliwa kama mhalifu wa kivita kutokana na mateso na machafuko anayowafanyia watu wake.

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Faysal Khabbaz Hamoui
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Faysal Khabbaz HamouiPicha: Reuters

Katika mkutano huo wa baraza la kutetea haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Balozi wa Syria katika Umoja huo Faysal Khabbaz Hamoui, alijiondoa katika mkutano akisema maazimio ya kimataifa yatailemaza Syria katika kununua dawa na mafuta kwa wananchi wake.

Hamoui amesema mataifa hayo lazima yawache kuchochea ghasia na kuwacha kutoa silaha kwa waasi nchini Syria.

Hata hivyo Marekani imesema huenda kundi la kigaidi la Al Qaeeda likachukua nafasi hii kutekeleza ghasia zaidi. Marekani imesema kwa sasa si wakati wa kuwapa waasi silaha nchini Syria.

Mwandishi Amina Abubakar

Mhariri Josephat Charo