1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda Champions League ikafanyiwa mabadiliko

25 Machi 2016

Ligi ya Mabingwa Ulaya huenda ikafanyiwa mageuzi mapana ambapo timu za hatua ya makundi zitagawanywa mara mbili na kuwekwa katika makundi mawili ya mfumo wa ligi za kawaida ili kuwezesha mechi zaidi baina ya timu kuu

https://p.dw.com/p/1IJz2
UEFA Champions League 2015-16 Ziehung Viertelfinale
Picha: picture-alliance/dpa/C. Brun

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Uingereza na Uhispania. Gazeti Uingereza la The Guardian likinuu duru za klabu moja kuu ya Premier League, limesema mabadiliko hayo yataunda kile kitakachokuwa ni ligi mbili ndogo. Gazeti la Mundo Deportivo la Uhispania pia lilizungumzia makundi mawili ya timu nane.

Chama cha mashirikisho la kandanda Ulaya – UEFA kimesema hakuna mapendekezo imara kwa sasa kwa sababu mabadiliko hayawezi kutekelezwa hadi mwanzoni mwa msimu wa 2018 na 19 kutokana na sababu za mikataba. Uamuzi wa kamati kuu ya UEFA unatarajiwa kufanywa mwishoni mwa mwaka huu.

Schweinsteiger huenda akacheza Euro 2016

Nahodha wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani Bastian Schweinsteiger ana nafasi ya kujumuishwa katika kikosi cha dimba la EURO 2016 licha ya kupata jeraha. Hayo ni kwa mujibu wa meneja wa timu Oliver Bierhoff.

Kiungo huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 31 alipata jeraha la mshipa wa goti wakati akiwa mazoezini Jumatano kabla ya michuano ya kirafiki ya England na Italia. Atakuwa mkekani kwa wiki kadhaa na Bierhoff anaamini kuwa atarejea kabla ya kuanza dimba la Uefa Euro 2016 nchini Ufaransa litakaloanza Mei 30 hadi Julai 10.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu