1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huku juhudi za kuumaliza zikiwa zinaendelea, Ukimwi umeendelea kuenea barani Afrika.

Scholastica Mazula2 Aprili 2008

Ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa tatizo kubwa Barani Afrika.

https://p.dw.com/p/DZRx
Esther Babalola mama mwenye umri wa miaka 38 na watoto wanne akimsubiri Daktari apate dawa za kurefusha maisha katika Kituo cha afya cha kuhudumia wagonjwa wa Ukimwi nchini Nigeria.2002.Picha: AP

Idadi kubwa ya watu wamekuwa wakipoteza maisha yao mapema kutokana matatizo ya kiuchumi yanalopelekea watu kujiingiza katika vishawishi vinavyosababisha maambukizi ya ugonjwa huo.

Akizungumza na mwandishi wetu Anaclet Rwegayura nchini Ethiopia mara baada ya kuzungumza na Mawaziri wa Fedha katika kikao chao cha Mwisho mjini Adis Ababa, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mapambano dhidi ya Ukimwi, UNAIDS, Peter Tiyot, amesema kwa mara ya kwanza wameweza kufanikiwa kupata takwimu sahihi za maambukizi ya ugonjwa huo barani Afrika.

Amesema kwa ujumla Afrika ina watu milioni mbili ambao wamekuwa wakitumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi.

Japo kuwa bado kuna watu milioni nne wanahitaji msaada wa dawa hizo, UNAIDS inaendelea na juhudi za kuhakikisha kwamba watu wote wanapata huduma hiyo.

Peter Tiyot, amebainisha kuwa huo ni mfano mzuri wa kuonyesha kwamba wamepiga hatua fulani katika juhudi za kupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa mfano katika nchi kama za Afrika Mashariki na Kusini ambako kumekuwa na maambukizi mapya kila wakati.

"Kwa hivyo hizi ni ishara nzuri kwamba tumepiga hatua, kwa hivyo sasa tunapaswa kuanza kufikiria upya kuhusu mkakati wa muda mrefu zaidi na kama mnavyofahamu UNAIDS itaendelea kuwepo kwa mingo na miongo kwa ajili ya vizazi vijavyo".

Amesema mbali na kwamba bara la Afrika lina watu milioni mbili ambao tayari wameshaanza kutumia dawa hizo za kurefusha maisha, lakini bado kuna haja ya kuweza kuliangalia kwa makini jambo hilo.

"UNAIDS, ingependa watu hao wote waendelee kuishi hata kwa miaka kumi, ishirini na hata thelathini, sana ni nani atawalipia gharama hizo, na ni nani ataandaa mpango huo? Ndilo jambo ambalo nimezungumza na Mawaziri wa fedha wa Afrika katika Kikao chao".

Amebainisha kwamba Mawaziri wa Fedha wa Afrika bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha wanachangia katika kupunguza ama kumaliza kabisa tatizo hilo.

Nchini Ethiopia, inakadiriwa kuwa kila mwezi watu elfu kumi hupata maambukizi ya Ukimwi na kila mwezi watu elfu nne kati yao hupata huduma ya dawa za kurefusha maisha kitu ambacho Bwana Tiyot anasema kinatia moyo.

Mbali na kwamba kati ya watu elfu kumi, kati yao elfu nne hupata dawa, bado hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya Nchi, hivyo watu wanapaswa kutambua kuwa Ukimwi hauna tiba lakini wanaweza kuuzuia usienee zaidi.

Amesema mbali na Ukimwi kuwa ndiyo moja ya sababu kuu ya vifo vingi barani Afrika, lakini pia Ugonjwa wa Malaria na Homa ya mapafu unahiji kudhibitiwa.

Kwa mujibu wa Takwimu, mwaka 2007, watu milioni moja nukta nane walifariki kutokana na Ukimwi Barani Afrika, Bwana Tiyot anasema vifo hivyo vinatokana na watu kutofuatilia matumizi ya dawa.

Nchi ambazo zinaorodheshwa kuwa watu wake wameathirika zaidi na Ugonjwa huo ni Swazland na Botswana pengine kutokana na idadi ya watu wake kuwa ndogo zaidi. Nyingine ni Afrika Kusini na Lethoto.

Nchi nyingine japokuwa zinajaribu kupambana na Ukimwi ni Malawi, Zambia, Msumbiji, Tanzania, Kenya na Uganda wakati kiwango cha waathirika katika nchi za Senegal, na Ivory Coast.

Ameonya baadhi ya watu ambao hujitangaza kwamba wanatibu Ukimwi pasipo kuthibitishwa kitaalamu, kuwa waache kwani hali hiyo inachangia watu kujisahau na ni kuudanganya umma.