1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huyu hapa ndiye Dominique Strauss-Kahn

19 Mei 2011

Wafaransa wengi wanamuheshimu mwanasiasa huyu mwenye mwendo wa madaha, ambaye ni mashuhuri kwa jina la mkato la DSK. Mwenyewe amewahi kusema kwamba ana udhaifu katika mambo matatu: pesa, wanawake na Uyahudi wake.

https://p.dw.com/p/11Jhl
Dominique Strauss-Kahn
Dominique Strauss-KahnPicha: dapd

Upande mmoja wa familia ya Dominiques Strauss-Kahn ni Mayahudi wenye asili ya Morocco, nchi ya Kaskazini mwa Afrika na iliyokuja kuwa miongoni mwa makoloni ya Hispania.

Lakini yeye mwenyewe alizaliwa mwaka 1949 katika eneo la Neuilly Sur-Sein, karibu na mji mkuu wa Paris, Ufaransa. Amekulia Morocco kabla ya kuhamia Monaco na kusomea baadaye mjini Paris.

Profesa huyo wa kiuchumi mwenye umri wa miaka 62, amekuwa pia akiwika katika jukwaa la kisiasa nchini Ufaransa kwa miongo miwili sasa.

Dominique Strauss-Kahn akiwa kizimbani
Dominique Strauss-Kahn akiwa kizimbaniPicha: AP

DSK, kama ulivyo umaarufu wake kwenye siasa za Ufaransa, alifuata nyayo za wazee wake na kuelemea mrengo wa kushoto. Alijiunga mapema na Chama cha Kisoshialisti ambacho mnamo mwaka 1971 kilikuwa nguvu muhimu ya mrengo wa kushoto uliokuwa ukiongozwa na Francois Mitterand.

Katika miaka ya '80 na '90 alikabidhiwa nyadhifa tofauti za kisiasa, hadi mnamo mwaka 1997 alipochaguliwa kuwa Waziri wa Uchumi, Fedha na Viwanda.

Yeye ndiye aliyetandika misingi ya ya Ufaransa kuweza kujiunga na sarafu ya euro. Wengi wanakiri kwamba Strauss-Kahn alifanikiwa kuunganisha mawazo yakinifu ya kiuchumi na yale ya ujamaa wa kidemokrasia. Kwa mfano, yeye ndiye aliyepunguza muda wa kufanya kazi kwa wiki na wakati huo huo kuanzisha utaratibu wa kubinafsishwa mashirika ya serikali.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: AP

Mnamo mwaka 1999, Strauss-Kahn alijiuzulu kwa tuhuma za kuhusika na rushwa, ingawa baadaye alitakaswa na tuhuma hizo. Baada ya kujizulu, DSK alikuwa akijishughulisha zaidi na kazi yake ya kusomesha kwenye vyuo vikuu.

Miongoni mwa mengineyo, alikabidhiwa jukumu la kusimamia chuo kikuu mashuhuri cha Institut d'Etudes Politiques (IEP), ambako binafsi ndiko alikosomea. Wakati huo huo akateuliwa kuwa mshauri wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo barani Ulaya (OECD).

Staruss-Kahn alirejea katika jukwaa la kisiasa mwaka 2001 na kuongoza kampeni ya uchaguzi ya Lionel Jospin mnamo mwaka 2002 alipopigania kuwa rais wa Ufaransa.

Akiwa mbunge, Strauss-Kahn alipigania sana masuala yanayohusu Ulaya na kuunga mkono ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa kama injini ya Umoja wa Ulaya. Yeye alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakiunga mkono katiba ya Umoja wa Ulaya iliyokataliwa na Ufaransa mnamo mwaka 2005.

Magazeti ya Ufaransa yakiandika taarifa za kashfa ya Strauss-Kahn
Magazeti ya Ufaransa yakiandika taarifa za kashfa ya Strauss-KahnPicha: picture alliance/dpa

Baada ya kukaa kwenye upande wa upinzani kwa miaka kadhaa, Strauss-Kahn akajitokeza kutaka kupigania kiti cha rais mwaka 2006 kwa tiketi ya chama chake cha Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto, lakini alishindwa na Ségolène Royal. Wakati huo, Strauss-Kahn alikuwa akifikiria umuhimu wa kuunda chama kipya cha mrengo wa kushoto.

Lakini kabla ya kufanya hivyo, akajikuta anateuliwa kuwa mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), akiwa amependekezwa na mpinzani wake wa kisiasa, Rais Nicolas Sarkozy.

Lakini mara tu baada ya kuchaguliwa kuongoza shirika hilo, IMF ikakafanya uchunguzi dhidi ya kiongozi wake mpya. Lengo lilikuwa kutaka kujua ikiwa bosi huyo alitumia vibaya madaraka yake na kumpendelea mtaalamu wa kike wa kiuchumi, Piroska Nagy.

Naggy, ambaye alisemekana kuwa na usuhuba na Strauss-Kahn, alikubali kupokea fidia mnamo Agusti mwaka 2008 na kuacha kazi yake kutoka IMF.

Baada ya Straúss-Kahn kuomba radhi wakati ule, baraza la shughuli za utawala likapiga kura kwa sauti moja kumruhusu kuendelea na kazi yake. Uchunguzi haukutoa ushahidi wowote wa madai ya kutumia vibaya madaraka yake.

Februari mwaka 2010, Strauss Kahn alisema katika mahojiano ya radio kwamba anaweza kuamua kutetea kiti cha rais kwa tiketi ya Chama cha Kishoshilisti dhidi ya Rais Sarkozy wa kutoka chama tawala cha UMP na, kwa hivyo, kuachana na IMF kabla ya wakati wake kumalizika.

Strauss-Kahn amemuowa mwandishi habari na mtangazaji wa televisheni, Anne Sinclair. Ana watoto wanne kutoka ndoa zake mbili za mwanzo. Ukiacha lugha yake ya Kifaransa, anazungumza pia kwa ufasaha Kiengereza na Kijerumani na pia ana ujuzi mzuri wa Kihispania na Kiarabu.

Mwandishi: Nicole Scherschun
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman