1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAAF: Urusi haijafanya mageuzi ya kutosha

11 Machi 2016

Shirikisho la Riadha la Kimataifa - IAAF limesema kuwa Urusi haijafanya mageuzi ya kutosha kuhusiana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu, ili kuondolewa hatua ya kupigwa marufuku dhidi yake

https://p.dw.com/p/1IBu7
England Sebastian Coe
Picha: imago/ZUMA Press

Rais wa IAAF Sebasian Coe amesema Urusi haipaswi kurejeshwa mashindanoni katika wakati huu. Kushiriki kwa Urusi katika michezo ya Olimpiki mjini Rio bado kuko katika hali ya ati ati, baada ya jopo kazi linalochunguza operesheni za nchi hiyo kubwa kimichezo ya kupambana na matumizi ya daa za kuongeza misuli nguvu kushindwa kutoa pendekezo thabiti wakati iliwasilisha ripoti yake kwa Baraza la Chama cha Kimataifa cha mashirikisho ya riadha – IAAF.

Coe amesema uamuzi wa ikiwa nchi hiyo itarejeshwa mashindanoni kwa wakati unaofaa kabla ya Michezo ya Olimpiki utafanywa na Baraza la IAAF mwezi Mei

Wiki iliyopita makala ya televisheni ya Ujerumani ARD ilisema Urusi imepiga hatua chache sana kuhusu mageuzi, kuwa makocha waliopigwa marufuku kutokana na sakata la matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu wangali wanahudumu nchini humo na maafisa waliochaguliwa karibuni kama sehemu ya juhudi za kuusafisha mchezo wa riadha wanawafichulia siri wanamichezo kabla ya kufanyiwa vipimo vya ikiwa wanatumia dawa hizo.

Meldonium Doping
Mchezaji wa Tennis Mrusi Maria Sharapova aligundulika kutumia dawa zilizopigwa marufuku aina ya MeldoniumPicha: picture-alliance/dpa/D. Sorokin

Masaibu ya Urusi na dawa zilizopigwa marufuku michezoni

Naibu waziri wa michezo wa Urusi amekosoa kiwango cha umakini unaoizunguka Urusi kuhusiana na suala la matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni. Akizungumza mjini Moscow katika mkutano kati ya wawakilishi wa wizara ya michezo ya Urusi na wabunge wa Urusi, Natalya Parshikova amesema matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu ni tatizo katika mataifa yote yanayoshiriki michezoni na kuwa suala hilo linatoa sababu “rahisi” ya kuishambulia Urusi hadharani

Matamshi ya Parshikova yamekuja baada ya tangazo la mapema wiki hii na nyota wa tennis Mrusi Maria Sharapova kuwa aligundulika kutumia dawa aina ya meldonium katika mashindano ya Australian Open mwezi Januari. Waziri huyo wa michezo amesema kila mchezaji lazima awajibishwe

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Gakuba Daniel