1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAAF yakosolewa kuhusu vipimo vya damu

10 Agosti 2015

Shirikisho la riadha la kimataifa – IAAF limekanusha madai kuwa kuna uzembe katika mchakato wake wa kufanya vipimo vya damu za wanariadha. Wadau wanataka hatua kali dhidi ya uovu huo

https://p.dw.com/p/1GCnr
Symbolbild Doping
Picha: Fotolia/gebai

Wanayasanzi wa Australia Michael Ashenden na Robin Parisotto wamedai kuwa mamia ya wanariadha walirejesha matokeo ya kutilisha shaka ya vipimo vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini.

Madai yao yalihusiana na uchunguzi wa data walizopewa zilizofichuliwa na gazeti la Uingereza Sunday Times na televisheni ya Ujerumani – ARD zilizokuwa na vipimo zaidi ya 12,000 kutoka kwa wanariadha 5,000 kati ya mwaka wa 2001 na 2012.

Shirikisho hilo limewataka watu hao wawili kutoa habari kwa WADA ikiwa wana ushahidi wowte kuhusu matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.

Kwa mujibu wa IAAF, madaktari hao wawili hawako katika nafasi ya kujua ni vipimo vipi vilivyowasilishwa kwa jopo huru kwa ajili ya kufanyiwa utathmimi au kufahamu ni kesi zipi zinaczochunguzwa. IAAF imesema zaidi ya wanariadha 60 wameadhibiwa kutokana na tabia hiyo mwaka wa 2009.

Kenia Läufer Kipchoge Keino
Mwanariadha mstaafu wa Kenya Kipchoge KeinoPicha: AP

Lakini Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki nchini Kenya, Kipchoge Keino amesema Shirika la Kimataifa la Kupambana na dawa zilizopigwa marufuku michezoni – WADA na Shirika la Kimataifa la Riadha – IAAF yanapaswa kuwajibika kutokana na madai ya kukithiri matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini katika mchezo wa riadha.

Wakuu wa riadha nchini Kenya wanapuuza madai hayo wakisema ni kampeni ya kuipaka tope nchi hiyo, lakini makocha na wanariadha wameonya kuwa taifa hilo lazima likabiliane na tatizo hilo linaloendelea kuongezeka ili kuilinda heshima na sifa yake ya muda mrefu.

Lucas Rotich ni mshindi wa mbio za Hamburg marathon hapa Ujerumani. Anasema "Ikiwa mtu atashinda mbio, akilini mwao kawaida watasema “wanariadha wa Kenya wanatumia dawa jambo ambalo sio zuri maana linamwathiri mtu binafsi kwa sababu ikiwa utashiriki mbio zozote hawatamwamini mtu kwa sababu akilini mwao wanafikiri kuwa anatumia dawa fulani".

Kama tu wengine wengi wanaowafunza wakenya, kocha Mholanzi Hugo van den Broek anahofia kuwa suala hilo litakuwa na athari kubwa "Miaka minne au mitano iliyopita, niliamini kuwa dawa zilizopigwa marufuku kamwe hazitumiki Kenya. Nilidhani kila mtu ni msafi lakini nimegundua kuwa suala hilo lipo na natumai na kuamini kuwa hakuna wanariadha wengi maarufu wanaohusika".

Wanariadha na makocha wanataka matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni lifanywe kuwa kosa la uhalifu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef