1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yasema Iran inafanya kazi ya kutengeneza silaha za nyuklia.

9 Novemba 2011

Shirika la atomiki la Umoja wa mataifa, IAEA limechapisha ripoti inayosema kuwa Iran inafanya kazi ya kutengeneza silaha za nyuklia. Shirika hilo limedai lina ushahidi kuhusu utafiti wa uundwaji wa silaha hizo.

https://p.dw.com/p/137CR
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad akiwa katika moja ya vinu vya nyukiliaPicha: AP

Shirika hilo la atomiki limesema katika ripoti yake kuwa lina wasiwasi mkubwa unaotokana na taarifa za kuaminika zinazoashiria kuwa nchi hiyo ya kiislamu imetekeleza shughuli zinazoambatana na kuunda silaha ya nyuklia.

Kwa kutumia taarifa kutoka vyanzo 10 vya mashirika ya upelelezi ya nchi za nje pamoja na taarifa zake, IAEA imeorodhesha yaliomo kwenye mpango huo wa Iran katika maeneo 12 ambayo yanagusia kila sehemu inayohitajika katika utengenezaji silaha.

Internationale Atombehörde IAEA
Mandhari ya ofisi za IAEA Vienna, AustriaPicha: dapd

Shirika hilo ambalo bodi yake huenda ikaamua kuishtaki Iran kwa baraza la usalama la Umoja wa mataifa wiki ijayo, imetoa wito kwa Iran kushirikiana nalo bila ya kuchelewa ili kutoa maelezo zaidi.

Kufuatia kutolewa ripoti hiyo, Marekani imesema kuwa ripoti hiyo imeonyesha kuwa Iran ilidanganya na imesema itatafuta kushinikiza mbinyo na pengine vikwazo vipya, lakini wachambuzi wanasema ripoti hiyo haitoshi kupata uungwaji mkono wa kutoka China na Urusi.

Kwa upande wake Urusi, imeshutumu uchapishaji wa ripoti hiyo ikisema itadidimiza matumaini ya majadiliano na Tehran, na huedna ikasitisha kufikiwa suluhu ya kidiplomasia.

Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema ripoti hiyo imekuwa chanzo cha kuongezeka upya wasiwasi kuhusu mpango wa Iran, hata pia kabla ya kuchapishwa kwake.

Urusi ambayo ni mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa, na iliyo na kura ya turufu, inajaribu kuzuia kuharibu uhusiano wake na Iran na wakati huo huo inajaribu kuonyesha umuhimu wake kwa mataifa ya magharibi katika diplomasia, inaitisha mpango wa hatua baada ya hatua, ambapo vikwazo vilivyopo dhidi ya Iran vitapunguzwa ili Iran kwa upande wake ithibitishe kuwa mpango wake huo wa nyuklia, ni wa amani kama inavyodai.

Miongoni mwa wengine waliotoa hisia zao kuhusu kuchapishwa ripoti hiyo, alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle aliyesema. "Iwapo suala hili litazidi makali, na kutajwa pia kwenye ripoti hii kwamba Iran inaendeleza mpango wake, basi Ulaya tutaidhinisha awamu nyengine ya vikwazo".


Ripoti hiyo imetolewa baada ya fununu za vyombo vya habari vya Israeli zilizoeleza kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulio dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran, jambo ambalo Urusi imelipinga mara kwa mara.

Israel kwa upande wake haikutoa tamko la mara moja baada ya kutolewa ripoti hiyo, huku msemaji wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu akieleza kuwa huenda ikafanya hivyo baada ya kuyapitia yaliomo ndani ya ripoti hiyo.

Hapo awali rais wa Israel, Shimon Peres, alionya kuwa shambulio dhidi ya Iran huenda linakaribia kutekelezwa, badala ya kutumia njia za kidiplomasia.

Mwandishi Maryam Abdalla/Afpe/Rtre/Dpae
Mhariri: Mohammed Khelef