1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yalalamika Kenya imekataa kushirikiana nayo

Admin.WagnerD7 Oktoba 2014

Waendesha mashitaka katika mahakama ya kimataifa inayoshughulikia uhalifu ya ICC wamewataka majaji wa mahakama hiyo kutoa uamuzi kuwa Kenya haijatoa ushirikiano unaostahili kuhusu kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenya

https://p.dw.com/p/1DRje
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Mwendesha mashitaka mwandamizi wa ICC Ben Gumpert ameliambia jopo la majaji watatu wanaoisikiza kesi dhidi ya Uhuru kuwa serikali ya Kenya haitaridhia kuwapa kile wanachokiomba kutoka kwao na ambacho kimeidhinishwa na mahakama hiyo kuombwa kutoka kwa serikali ya Kenya.

Gumpert amesema kutokana na mantiki hiyo,iwapo mahakama hiyo itaridhishwa na hoja za upande wa mashitaka, basi inapaswa kutangaza kuwa serikali ya Kenya imekataa kushirikiana nao.

Kenyatta ndiye Rais wa kwanza ICC

Majaji wa ICC wanaendesha vikao vya siku mbili kuanzia leo ya kuamua muelekeo wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili Uhuru Kenyatta, kiongozi wa Kenya ambaye ni rais wa kwanza aliye madarakani kukubali kwa hiari yake kufika mbele ya mahakama hiyo kukabiliwa na mashitaka.

Mwendesha mkuu wa mashitaka ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mkuu wa mashitaka ICC Fatou BensoudaPicha: Bas Czerwinski/AFP/GettyImages)

Hata hivyo kesi hiyo imekumbwa na hatari ya kuporomoka huku ikiahirishwa mara kadhaa kutokana na madai kuwa mashahidi wanatishiwa,wengine wamejiondoa na kukataa kutoa ushahidi dhidi ya Uhuru na madai pia ya serikali ya Kenya kukataa kushirikiana na ofisi ya mwendesha mashitaka.

Iwapo majaji wa ICC wataamua kuwa Kenya imekataa kushirikiana na mahakama hiyo,suala hilo litawasilishwa mbele ya mkutano wa nchi wanachama waliotia saini mkataba wa Roma uliopelekea kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Wachambuzi wanasema kuwasilishwa kwa malalamiko hayo ya ICC mbele ya mkutano mkuu wa nchi wanachama wa mkataba wa Roma ujulikanao kwa kifupi ASP hautakuwa na matokeo yoyote makubwa mbali na kulaani tu kwani itakuwa ni kama kuipiga Kenya kofi katika kifundo cha mkono.

Kenyatta yuko njiani hii leo kuelekea Hague ambako anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo hapo kesho katika kile majaji wa ICC wamekitaja hatua muhimu katika kesi inayomkabili.

Kenya ina urasimu wa hali ya juu

Akizungumza kwa niaba ya Kenya mkuu wa sheria wa Kenya Githu Muigai amesema leo nchi yake kama nchi nyingine ile ina urasimu wa hali ya juu na kwamba ameziandikia taasisi mbali mbali nchini humo kutaka kupewa taarifa zinazohitajika na ICC na wako tayari kufanya hivyo.

Mkuu wa sheria wa Kenya Githu Muigai
Mkuu wa sheria wa Kenya Githu MuigaiPicha: picture alliance/dpa

Rais Kenyatta mwenye umri wa miaka 52 anakabiliwa na mashitaka matano ICC kwa madai ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo kiasi ya watu 1,200 waliuawa na wengine kiasi ya laki sita kuachwa bila makaazi.

Kiongozi huyo wa Kenya ameshawahi kufika mbele ya mahakama hiyo awali lakini hakuwa amechaguliwa kuwa rais. Majaji walitisha kikao hicho maalum na Kenyatta baada ya kesi dhidi yake kuahirishwa kutokana na waendesha mashitaka kukiri hawana ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi hiyo.

Mwendesha mkuu wa mashitaka Fatou Bensouda alitaka kesi hiyo iahirishwe kwa muda usiojulikana akisema Kenya imekataa kushirikiana naye kwa kukataa kumpa hati za kuonyesha mawasiliano ya simu,ya kodi na uwezo wa Kenyatta wa kifedha.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman