1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yamfutia kesi ya mauaji William Ruto

5 Aprili 2016

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imefuta kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto Jumanne (05.04.2016) ikisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa ushiriki wake katika vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007/2008.

https://p.dw.com/p/1IPs7
Niederlande Kenia Anhörung zu Gewalt nach Präsidentenwahl in den Haag William Samoei Ruto
Picha: dapd

Jaji aliyesimamia kesi hiyo alisema yumkini sababu ya kukosekana kwa ushahidi ilikuwa uingiliaji wa mashahidi na ushawishi wa kisiasa. Tangazo la mahakama hiyo linaonyesha mara ya pili ambapo mahakama ya ICC imekubali kushindwa katika jitihada zake za kuwashtaki wanaodaiwa kupanga na kufadhili vurugu zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 na kuwalazimisha wengine 600,000 kuyakimbia makazi yao nchini Kenya.

Naibu Rais William Ruto alishtakiwa sambamba na mtangazaji wa redio Joshua Sang, kwa makosa ya mauaji, kuwalazimisha watu kuyahama makaazi yao na utesaji kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ushiriki wao katika vurugu hizo. Kesi dhidi ya Sang pia ilihitimishwa siku ya Jumanne.

Televisheni za nchini Kenya ziliwaonyesha wawili hao wakipunga mikono hewani kusherehekea ushindi huku wafanyakazi wa ofisi ya Ruto wakimkumbatia kumpongeza. Picha hizo pia ziliwaonyesha mamia ya watu katika mji wa Ruto wa Eldoret wakishangilia.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akifurahia jambo na naibu wake Ruto ambae amekuwa huru baada ya kesi dhidi yake kufutwa na ICC.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akifurahia jambo na naibu wake Ruto ambae amekuwa huru baada ya kesi dhidi yake kufutwa na ICC.Picha: Reuters/Thomas Mukoya

'Ni thibitisho la kutokuwa na hatia!

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema kufungwa kwa kesi hiyo ni uthibitisho kwamba naibu wake pamoja na mwandishi habari Sang hawakuwa na hatia.

"Ni bahati mbaya kwamba ICC iliwapa Wakenya matumaini ya uongo, na matokeo yake imesababisha ukataji tamaa mkubwa. Tutafanya kila kitu kuwafidia Wakenya pale mahakama hii ilipowaangusha," alisema Kenyatta katika taarifa.

Kesi dhidi ya Kenyatta katika mashtaka sawa na hayo ilivunjika Desemba 2014 baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa kulikuwepo na uingiliaji katika mashahidi, na kukosa ushirikiano kutoka kwa utawala mjini Nairobi.

Wakati huo, mwendesha mashtaka mkuu Fatou Bensouda, aliilaumu Kenya kwa kuzuwia uchunguzi wake na kuitaja siku hiyo kuwa ya giza katika utoaji haki dhidi ya uhalifu wa kimataifa. Wakenya watatu wameshtakiwa kwa kuingilia mashahidi.

Kuvunjwa moyo kwa waathirika

Wakili anayewawakilisha waathirika wa machafuko hayo katika mahakama ya ICC Wilfred Nderitu, alisema kufutwa kwa kesi hiyo kabla ya kutolewa hukumu lilikuwa jambo la kuvunja moyo, na kuwataka waendesha mashtaka kukata rufaa.

"Hakuna shaka kwamba uamuzi huu utakuja kama jambo la kuvunja moyo kwa waathirika," alisema Nderitu wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi. "Ni matumaini yangu kwamba waendesha mashtaka watakata rufaa."

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda.
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda.Picha: Reuters

Elizabeth Evenson, wakili mwandamizi wa kimataifa kutoka shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, alisema kushindwa kwa waendesha mashtaka kuwashtaki waliopanga uhalifu dhidi ya Wakenya, "kunawaacha waathirika wakiwa wamenyimwa haki na msaada wanavyovihitaji."

Alisema kesi ya Ruto itakumbukwa kwa juhudi zilizoripotiwa juu ya kuwahonga mashahidi.

Mchambuzi wa masuala ya kimataifa kutoka Kenya Agina Ojwang aliiambia DW katika mahojiano kuwa kutokuwa makini kwa ICC mwanzoni mwa kesi hiyo - katika kuwalinda mashahidi ndiyo kumechangia kesi hiyo kushindwa, ambapo alitaja kuuawa kwa baadhi ya mashahidi hao katika mazingira ya kutatanisha, na wengine kupotezwa kabisa.

Mashtaka yanaweza kufunguliwa upya

Katika uamuzi wao siku ya Jumanne, wajumbe wawili wa jopo la majaji waliamuru kesi hiyo ifutwe, ingawa walisema mashtaka yanaweza kufunguliwa tena ikiwa kutakuwa na ushahidi wa kutosha.

Kulingana na taarifa ya mahakama, jaji msimamizi Chile Eboe-Osuji alisema kesi hiyo inaweza kuelezwa na matukio yalioonyesha kutiwa madoa mchakato wa mashtaka kwa kuingilia mashahidi na ushawishi wa kisiasa, ambavyo vilionekana kuwatishia mashahidi.

Majaji wa rufaa watoa hukumu mwezi Februari kwamba matamshi yaliyotolewa na mashahidi watano ambao baadaye walibadilisha maelezo yao au kukataa kutoa ushahidi dhidi ya Ruto na Sang, yasingeweza kutumiwa kama ushahidi, uamuzi ambao huenda uliharakisha kuvunjika kwa kesi hiyo.

Mwandishi habari Joshua Arap Sang, alieshtakiwa sambamba na naibu rais Ruto.
Mwandishi habari Joshua Arap Sang, alieshtakiwa sambamba na naibu rais Ruto.Picha: picture-alliance/dpa

Awali, waendesha mashtaka wa ICC waliwashtaki Wakenya sita kwa makosa yanayohusiana na ghasia za baada ya uchaguzi, na mashtaka dhidi ya watu hao wote sita yameondolewa.

Waathirika wataka fidia

Zephania Mwangi, ambaye babu yake alikatwa hadi kufa na kundi la watu wenye hasira katika eneo la mabanda lililoshuhudia kuripuka kwa vurugu baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, alisema mahakama ya ICC inapaswa kuwafikiria waathirika.

"Kama mtu alipoteza mali au ndugu, wanapaswa kufidiwa angalau ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida," alisema kabla ya kuchapishwa kwa uamuzi wa majaji wa mahakama hiyo.

Madai ya uingiliaji mkubwa dhidi ya mashahidi unatilia mkazo tatizo kubwa linaloikabili mahakama hiyo, iliyoundwa kwa lengo la kuwashtaki washukiwa wanaochukuliwa kuhusika na unyama. Hilo linamaanisha kuwa wakati mwingine kuwashtaki wanasiasa na kutegema polisi wao na vyombo vingine vya usalama kwa kutoa ushirikiano.

Mwandishi. Iddi Ssessanga/ape,afpe,rtre.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo