1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yatiwa shaka na serikali ya Kenya

30 Mei 2011

Ujumbe wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu unawasili Kenya kukutana na Serikali kujadiliana ulinzi kwa mashahidi wa kesi inayowakabili washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

https://p.dw.com/p/RQmj
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha wa Kenya, Uhuru KenyattaPicha: AP

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Louis-Moreno Ocampo, ameonesha kuwa na shaka na namna serikali ya Kenya inavyolishughulikia suala hili.

"Tutatathmini mpango wa kuwapa ulinzi mashahidi na pia kupata ufafanuzi wa msimamo wa serikali ya Kenya juu ya swala zima la ghasia zilizozuka a baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007." Amesema Ocampo.

Ocampo amesema kwamba licha ya kujitolea kwa Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kushirikiana na Mahakama ya ICC, kuna baadhi ya maafisa wakuu serikalini wanaohujumu juhudi za mahakama hiyo kutekeleza haki kwa waathirika wa ghasia za baada ya uchaguzi.

Mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka, alikuwa kwenye ziara katika mataifa wanachama wa Muungano wa Afrika kuyashawishi kuunga mkono azma ya Kenya kuziondoa kesi za washukiwa sita wa ghasia za baada ya uchaguzi kutoka mahakama ya ICC.

"Niko katika ziara wakati huu kwa niaba ya Rais Mwai Kibaki. Lengo la ziara hii ni kujaribu kuiondoa Kenya kutoka kwa ICC." Alisema wakati huo Musyoka.

Lakini Ocampo ameishutumu hatua hiyo akisema kuwa inahujumu kesi hiyo

"Wanafanya kampezi za kusimamisha kesi hiyo. Hii sio tu ishara mbaya, lakini pia inaendeleza hofu ya kutishia usalama wa mashahidi walio tayari kutoa ushahidi wao na kuhujumu uchunguzi wa kitaifa na kimataifa." Amesema Ocampo.

Maafisa hao wa ICC wanaowasili leo (30.05.2011) nchini Kenya wanatarajiwa kushauriana na viongozi wa serikali na kisha kuandaa mkutano na waandishi wa habari hapo kesho saa 6:00 mchana.

Ocampo amesema ofisi yake inafanya kila juhudi kuhakikisha haki inapatikana kwa wahanga kama ilivyokubaliwa kwenye Ajenda ya Nne ya Mkataba wa Amani uliotiwa saini na pande zote mbili za serikali ili kuzuia machafuko mengine kwenye chaguzi zijazo.

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Othman Miraji