1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yatoa waranti wa kukamatwa Gaddafi

28 Juni 2011

Mahakama ya uhalifu wa kivita ya The Hague nchini Uholanzi, leo hii imetoa waranti ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi huku waasi nchini Libya wakijaribu kusonga mbele km 80 kufika mji mkuu wa Tripoli

https://p.dw.com/p/11kMX
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Luis Moreno-Ocampo
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Luis Moreno-OcampoPicha: picture alliance/dpa

Mahakama imeidhinisha waranti ya kukamatwa kwa Gaddafi, mwanawe Saif Saif al-Islam na Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Libya, Abdullah al-Senussi kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu.

Waendesha mashitaka wa ICC wanawatuhumu kwamba wamehusika na mauwaji ya waandamanaji walionzisha vuguvugu Februari mwaka huu la kuondoa madarakani utawala wa Gaddafi ulidumu kwa takribani miaka 41 sasa.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Sanji Mmasenono Monageng amesema kwa uhakika na bila ya shaka yeyote Gaddafi anadhibiti kila kitu nchini Libya, ikujumuisha jeshi.

Gaddafi Clan Saif al-Islam Gaddafi
Mtoto wa Gaddafi, Saif al-IslamPicha: AP

Aliongeza kwa kusema kwamba Gaddafi na Saif al- Islam kwa pamoja walipanga na kutekeleza mpango wa kuwazuia na kuzima kwa namna yeyote ile maandamano ya raia wa nchi hiyo dhidi ya utawala wake.

Na kwamba al-Senussi alitumia madaraka yake yake kuamuru mashambulizi yaliyotokea.

Serikali ya Gaddafi imekana kuwalenga raia na kuuhushtumu Umoja wa Kujihami NATO ambao ndege zake zinaendelea na operesheni za anga nchini humo kwamba zinafanya maangamizi kwa niaba ya Waasi.

Hatua ya kutolewa kwa waranti wa kukamatwa Gaddafi imepokewa vyema na Serikali ya Uingereza, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo, William Hague, amesema viongozi wengine walio katika utawala wa kiongozi hiyo wanapaswa kumtekelekeza.

Waziri huyo amesema watu hao wanatuhumiwa kufanya uhalifu dhidi ya binadamu, kwa hivyo wanapaswa kupandishwa kizimbani. Aidha ametoa wito kwa serikali ya Libya kutoa ushirikiano katika kufanikisha uchunguzi.

Nayo Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema hatua ya ICC inaonesha dhahiri kwamba muda unamtupa mkono Gaddafi, huku ukitangaza kuongeza kumbana zaidi kiongozi huyo wa Libya.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema hatua hiyo inaongeza mgawanyiko miongoni mwa waliomo katika utawala wa Gaddafi.

Hatua hiyo imezusha nderemo na vifijo huko mjini Benghazi, ambapo msemaji wa Baraza la Mpito la Waasi, Jalal al- Galal, amesema wana furaha kupita kiasi.

Amesema dunia imeungana kusheherekea kwa kumshitaka Gaddafi kwa uhalifu alioufanya.

Unruhen in Libyen
Wapiganaji waasiPicha: picture alliance/dpa

Kwa upande wao, wapiganaji waasi waliopo maeneo milimani, kusini mashariki mwa mji wa Tripoli, wamepiga hatua kubwa kwa wiki kadhaa na kuufikia mji wa Bir al-Ghanam ambapo hivi sasa wanakabiliana na vikosi vya Gaddafi kuweza kuudhibiti mji huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waasi hao, hivi sasa wapo umbali wa kilometa 30 kufika mji mkuu wa nchi hiyo wa Tripoli ambao ndio ngome ya Gaddafi.

Mwandishi: Sudi Mnette/DPA/RTR

Mhaariri: Miraji Othman