1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wakimbizi duniani yaongezeka - UNHCR

19 Juni 2017

Idadi ya watu walioyatoroka makaazi yao duniani ilifikia milioni 65.6 mwaka jana wakati ambapo mzozo mpya mkuu wa wakimbizi uliibuka Sudan Kusini na haya ni kwa mujibu wa UNHCR.

https://p.dw.com/p/2exRk
Südsudan Flüchtlinge
Wakimbizi wa Sudan KusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Huku takwimu hizo za Shirika hilo la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi zikionesha idadi mpya, kasi ya wakimbizi wanaotoroka ilipungua kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka mingi mwaka 2016.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, Filipo Grandi lakini ameonya, huko kupungua kasi ya wakimbizi wanaotoroka nchi zao, hakustahili kuonekana kama mwelekeo mzuri, akisema hiyo idadi ya milioni 65.6 ni kubwa hata kushinda idadi ya watu wa Uingereza.

Idadi hiyo inaashiria ongezeko la watu 300,000 kutoka mwishoni mwa mwaka 2015, lakini imezidi idadi ile iliyokuwa mwishoni mwa mwaka 2014 kwa milioni sita.

Wakimbizi wengi wanatoka mataifa yaliyo katika machafuko

Machafuko ya Sudan Kusini yamekuwa chanzo cha mzozo wa dunia unaokuwa kwa haraka unaochangia kwa watu kutoroka makaazi yao. Idadi ya Wasudan Kusini waliotorokea nchi nyengine iliongezeka kwa asilimia 64 na kufikia milioni 1.4 katika nusu ya pili ya mwaka jana. Idadi kamili kwa sasa imefikia karibu milioni 1.9 huku watu wengine milioni 2 wakiwa wakimbizi ndani ya nchi yao.

Mittelmeer - Flüchtlinge – Boot
Wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wakiwasili Lesbos, UgirikiPicha: Getty Images/AFP/A. Messinis

"Ni jambo la kushangaza kuona jinsi mataifa yaliyoanguka ama mataifa yaliyozongwa na machafuko yanayochangia kwa watu kutoroka kwa lazima," alisema Grandi, "asilimia 54 ya wakimbizi wanatokea nchi tatu zilizoathiriwa pakubwa na suala la wakimbizi nchi hizo zikiwa Syria, Afghanistan na Sudan Kusini. Na unapotazama wakimbizi wa ndani ya nchi zao, wanatokana na machafuko. Thuluthi tatu ya wakimbizi hao milioni 40 wanatoka katika nchi 10 tu."

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mwishoni mwaka 2016, kulikuwa na wakimbizi wa ndani ya nchi zao milioni 40.3 duniani, idadi hiyo ikiwa chini kidogo na ile ya milioni 40.8 mwaka 2015 huku Syria, Iraq na Colombia zikichangia idadi kubwa ya wakimbizi hao.

Watu zaidi ya milioni 5 wametoroka Syria tangu kuanza kwa mzozo miaka 6 iliyopita

Watu wengine milioni 22.5 walisajiliwa kama wakimbizi mwaka jana, nusu yao wakiwa ni watoto, jambo ambalo ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema ni ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa.

UNHCR Flüchtlinge Grenze Ungarn Kroatien
Wakimbizi wakimbia baada ya kuvuka mpaka wa CroatiaPicha: picture alliance/AP Photo/P.David Josek

Mzozo wa Syria pekeyake ambao umedumu kwa miaka 6, umewafanya watu milioni 5.5 kutafuta usalama katika nchi zengine, ikiwemo yaidi ya watu 800,000 mwaka jana pekee, jambo linaloifanya nchi kuwa nchi inayotoa wakimbizi wengi duniani.

"Natumai tumejifunza kutokana na yaliyopita. Natumai pia kwamba Wasyria hawajasahaulika kutokana na mipaka iliyofungwa Ulaya na kwengineko, kwa sababu hawaingii nchi nyingine kwa wingi kama hapo awali," alisema Grandi. "Huo mzozo wa wakimbizi bado upo nasi na bado tunastahili kuuzungumzia mpaka kuwe na fursa ya kuutatua, natumai kupitia kuwarejesha wakimbizi hao makwao."

Mkuu wa UNHCR barani Afrika Valentin Tapsoba anasema, hakuna mzozo wa wakimbizi unaomtia wasiwasi duniani sasa hivi kama ule wa Sudan Kusini.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo