1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliofariki Duisburg yafikia 21

Thelma Mwadzaya29 Julai 2010

Idadi ya waliopoteza maisha yao katika msongamano kwenye tamasha la Love-parade la wikendi imefikia 21.

https://p.dw.com/p/OX4T
Purukushani zilizotokea kwenye tamasha la LoveparadePicha: AP

Kulingana na maafisa wa serikali,mwanamke mmoja aliye na umri wa miaka 25 amefariki kwasababu  ya majeraha  aliyoyapata wakati wa purukushani hizo  zilizotokea mwishoni mwa wiki  iliyopita.Ziadi ya watu 500 walijeruhiwa.Waziri wa mambo ya  ndani  wa  Mkoa  wa North-Rhein  Westphalia ,Ralf Jäger amewalaumu waandaji  wa tamasha  hilo kwa kutowajibika.

Kulingana na kiongozi huyo,lango  kuu  la eneo la tamasha lilifunguliwa kuchelewa jambo  lililosababisha  msongamano.Takwimu za  polisi zinaonyesha kuwa kiasi cha watu laki nne walikuwako kwenye eneo la tukio.Ibada  maalum ya ukumbusho imepangwa kufanyika  mjini Duisburg ifikapo Jumamosi.Rais wa Ujerumani Christian  Wulff na Kansela Angela Merkel wanatarajiwa kuhudhuria shughuli  hiyo.    

p>Eneo lilikuwa dogo

NO FLASH Loveparade Massenpanik Duisburg Absperrung Gitter
Eneo la mkasa wa mwishoni mwa wiki iliyopita,DuisburgPicha: AP

Kwa  sasa  wachunguzi wanayatathmini mazingira yaliyosababisha maafa hayo  ambayo huenda yalichangiwa na kutowajibika.Kulingana na  Mwendesha mashtaka mkuu wa  mji wa Duisburg,Rolf  Haferkamp,mahakama itaichunguza mipango ya usalama iliyoandaliwa pamoja na idadi ya  waliohudhuria  tamasha iliyopindukia.Bwana  Haferkamp alifafanua kuwa  uchunguzi huo huenda ukachukua muda wa wiki  kadhaa au hata miezi.  

Uongozi wa mji huo pamoja na waandalizi wamekosolewa kwa kuruhusu idadi kubwa ya watu kuingia  katika eneo dogo kulikofanyika tamasha  lenyewe.Kiasi  cha watu milioni 1.4 wanaripotiwa kukusanyika kwenye eneo hilo la tukio  kinyume na idadi iliyoruhusiwa ya alfu 250.Wakati yote hayo yakiendelea,tetesi zimejitokeza kuwa uongozi wa mji  uliziupuuza kauli maafisa wa polisi za kutoliandaa tamasha hilo la muziki wa  Rock mjini humo kwasababu za kiusalama.Katika taarifa yake,Meya wa Duisburg Adolf Sauerland,alisema iwapo uongozi wa mji haukuwajibika,basi utachukua dhamana.

Uchunguzi kamili

Kwa sasa  Meya huyo  wa Duisburg ameusisitizia  umuhimu wakufanya  uchunguzi kamili kwanza hata anapoandamwa na madai ya  kumtaka ajiuzulu.    

Mkasa   huo wa Jumamosi ulitokea karibu  na lango la pekee la kuingia kwenye uwanja wa tamasha.Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa  watu zaidi ya 500 walijeruhiwa.Imebainika  kuwa hilolimechangia  pakubwa katika mkasa huo.Kwa mujibu  wa mtaalam mmoja wa usalama anayesimamia kampuni moja ya inayotoa huduma  za usalama  kwenye matamasha,lilikuwa   jambo la kushangaza kwa uongozi wa mji  kuidhinisha kibali cha kuandaa shughuli hiyo.   

Flash-Galerie Loveparade Duisburg 2010
Shamrashamra kabla ya mkasa kutokeaPicha: picture-alliance/dpa

Kuna tetesi   kuwa uongozi wa mji uliupuuza  wito wa maafisa  wa polisi wa  kutowapa vibali waandalizi wa tamasha hilo  ambalo ni moja ya  matamasha  makubwa ya muziki  aina ya Rock  kwasababu mji wa  Duisburg haukuwa na uwezo wa kupambana  na dharura  ya aina hiyo.7 kati  ya watu hao  waliofariki wanaripotiwa   kutokea mataifa ya Austria,Italia,Uholanzi,China,Bosnia  na Uhispania.

Masuali yote hayo  yameulizwa  na  hata Waziri Mkuu wa jimbo la North-Rhein  Westphalia Hannelore Kraft amesema  kuwa  mipango ya   usalama haikuwa imeandaliwa vizuri.

Tamasha la Loveparade lilianzia  katika mji mkuu  wa Berlin ulio na jumla  ya  wakazi milioni 3.4  na mwaka   2006 lilifanyika kwenye uwanja mkubwa.Mji  wa Duisburg  una  jumla  ya wakazi laki  5.    

Mwaka uliopita uongozi wa mji  wa Bochum ulilazimika kulifuta tamasha  hilo kwasababu  za kiusalama zilizotolewa  na   polisi wa eneo  hilo.