1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Urusi waapa kukabiliana na ugaidi

29 Machi 2010

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi ahutubia taifa, aapa kukabiliana na Magaidi.

https://p.dw.com/p/MhCq
Maafisa wa Polisi washika doria karibu na eneo la miripuko, Moscow.Picha: AP

Miripuko ya leo asubuhi mjini Moscow yametajwa kama mbaya zaidi kutokea katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Wizara inayoshughulikia mambo ya dharura imethibitisha kwamba watu 38 waliuawa. Katika mripuko wa kwanza watu 24 waliuawa na 20 kujeruhiwa katika kituo cha Lubyanka na wengine 14 walipoteza maisha yao na 15 kujeruhiwa katika mripuko wa pili karibu na bustani la utamaduni.

Maafisa wa idara ya ujasusi ya Urusi, FSB wamesema waripuaji hao wawili wanawake waliojitoa mhanga walikuwa na mabomu ya uzito wa kilo moja na nusu na kilo tatu .

Russland Zahlreiche Tote bei U-Bahn-Explosionen in Moskau‎ Flash-Galerie
Helikopta ya wizara ya mambo ya dharura kando ya bustani la utamanduni, Moscow.Picha: AP

Mamia ya waokoaji walifika katika maeneo ya mikasa yanayotajwa kama mbaya zaidi tangu mwaka wa 2004 wakati mwanamgambo wa Kichechen aliporipua bomu katika kituo cha treni na kuwauwa watu 41 na kuwajeruhi wengine 250.

Picha za televisheni nchini Urusi zilionyesha vituo vya treni chini ya ardhi zikifuka moshi na waathiriwa walitiririkwa na damu. Kufikia sasa hakuna kundi lolote lililojitokeza kupanga miripuko hiyo lakini wachunguzi wanawatuhumu wanachama wa kundi la wanamgambo wa kaskazini wenye msimamo mkali wa Kiislamu. Meya wa mji wa Moscow, Juri Luschkov alikiri kwamba miripuko hiyo ilikuwa imepangwa.

Kituo cha Lubyanka kiko karibu na makao makuu ya shirika la ujasusi la FSB lililochukua nafasi ya lile la KGB.

Russland Zahlreiche Tote bei U-Bahn-Explosionen in Moskau‎ NO FLASH
Polisi Mjini Moscow katika jitihada za uokoaji.Picha: AP

Mwendesha mashtaka mjini Moscow alisema waripuaji hao wa kujitoa mhanga walikuwa wamebeba mambomu hayo lakini bado hawajadhibitisha kama yaliripuriwa kwa kutumia mbinu ya kisasa inayohusisha simu ya kiganjani.

Shirika la habari la Novosti limeripoti kwamba wachunguzi walipata bomu lingine ambalo halikuwa limeripuka karibu na eneo la mikasa.

Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev aliyeongoza dakika moja ya ukimya kuwakumbuka waliowawa, awali alitoa hotuba kwa taifa na aliapa kupiga vita ugaidi.

Waziri mkuu wa Urusi, Vladmir Putin alikatiza ziara yake ya Siberia na alitoa wito kwa mashirika ya ujasisi nchini humo kufanya kazi kwa pamoja kukabiliana na ugaidi.

Kati ya viongozi waliotuma risala zao za rambirambi ni Rais Barack Obama wa Marekani, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Mawaziri wakuu Gordon Brown wa Uingereza na Manmohan Singh wa India , viongozi wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya kujihami ya NATO.

Mwandishi, Peter Moss/Reuters/AFP/AP/DPA

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed