1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouwawa Nairobi huenda ikaongezeka

MjahidA24 Septemba 2013

Wingu la simanzi bado limetanda Kenya kufuatia shambulio la kigaidi lililofanywa katika jengo la maduka ya kifahari la Westgate jijini Nairobi. Zaidi ya watu 60, wameuwawa na idadi hiyo huenda ikaongezeka.

https://p.dw.com/p/19mz4
Waathirika wa shambulizi la Westgate
Waathirika wa shambulizi la WestgatePicha: Reuters

Hadi kufikia asubuhi ya hivi leo, vikosi vya maafisa wa kulinda usalama vilikuwa vimelizunguka eneo la tukio huku shughuli za upekuzi wa jengo hilo zikiwa bado zinaendelea.

Shambulio hilo lililotokea Jumamosi mchana na hadi kufikia leo Jumanne bado maafisa wa usalama wanapambana na magaidi hao.

Tukio hili limewashtusha sana wakenya na kuwaacha na majonzi makubwa. Kulingana na taarifa kutoka kwa serikali ya Kenya mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Awoonor, aliye na umri wa miaka 78 ni miongoni mwa waliouwawa katika shambulizi hilo.

Askari polisi wakabiliana na Magaidi
Askari polisi wakabiliana na MagaidiPicha: Reuters

Hata hivyo, wanajeshi wa Kenya wakishirikiana na maafisa wa usalama kutoka nchini Israel, Uingereza na Marekani walifanya kila juhudi za kuwaokoa mateka wanaoshikiliwa na magaidi hao.

Inaarifiwa kuwa zaidi ya watu wapatao 1,000 walinusurika baada ya kuokolewa na walinda usalama katika shambulizi hilo siku ya Jumamosi.

Waathiriwa wazungumzia masaibu yaliowakuta

Bi. Mary Anyango, alikuwa miongoni mwa manusura waliokolewa na maafisa wa usalama.

Kulingana na Bi Mary risasi risasi zilisikika kila mahali. " Tulijaribu kukimbia lakini wapi? mwishowe nilitambaa hadi nikafika katika ofisi yangu ambapo nilijifungia hadi wakati polisi walipofika na kuniokoa," Alisema Bi Mary Anyango.

Bw. Wilson Kimani, ni mmoja wale walio na jamaa walioathiriwa na janga hilo.

Mwandishi wa DW Reuben Kyama alikutana naye nje ya hospitali ya MP Shah jijini Nairobi, na kumueleza jinsi mjomba wake alivyojeruhiwa kwenye shambulizi hilo kwa kupigwa risasi jichoni na mkononi.

Watu wakimbilia usalama wao wakati wa tukio
Watu wakimbilia usalama wao wakati wa tukioPicha: Reuters

Wakati huo huo raia watatu wa Uingereza, wanawake wawili raia wa Ufaransa, watu wawili kutoka Canada akiwemo mwanadiplomasia mmoja, mwanamke mmoja raia wa China, wahindi wawili, raia mmoja wa Korea Kusini na mwanamke mmoja wa Uholanzi ni miongoni mwa waliouwawa katika shambulizi hilo.

Ruto asema usalama utaendelea kuimarishwa Kenya

Akizungumza na wanahabari makamu wa rais wa Kenya William Ruto alilaani vikali mashambulizi hayo na kusema kwamba serikali itafanya kila iwezalo kuwatia mbaroni wale waliohusika na tukio hilo la kinyama.

Katika hospitali ya MP Shah moja ya hospitali ambako majeruhi wanapoke matibabu, madaktari huko wamesema wamepokea zaidi ya majeruhi 120 na hadi kufikia jana jioni kulikuwepo na miili 19 iliohifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Makamu wa rais William Ruto
Makamu wa rais William RutoPicha: picture alliance / Kyodo

Takwimu za serikali zaashiria kuwa watu wapatao 62 walifariki ilhali ziadi ya wengine 165 walijeruhiwa.

Mwandishi:Reuben Kyama

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman