1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watoto wanajeshi yafikia zaidi ya laki mbili

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP12 Februari 2009

Ulimwengu waadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya watoto kama wanajeshi.

https://p.dw.com/p/Gszj
Baadhi ya zaidi ya watoto 163 waliotekwa nyara na waasi jamuhuri ya kidemocrasia ya Congo.Picha: AP

Hii leo ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya watoto kama wanajeshi, shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limesema kutokana na ongezeko la migogoro duniani idadi ya watoto wanajeshi ni imefikia zaidi ya laki mbili.



Katika jimbo la darfur nchini Sudan zaidi ya watoto elfu sita wengine wakiwa wako chini ya umri wa miaka 11 wameingizwa kwa lazima katika vikosi vya waasi na majeshi ya serikali. Watoto hao wamekuwa wakionekana wakibeba silaha, licha ya sheria za Sudan na makubaliano ya kimataifa kupiga marufuku matumizi ya watoto jeshini katika maeneo yanayokabiliwa na migogoro.


Msimamizi wa shirika la UNICEF nchini Sudan Ted Chaiban, amesema ana ushahidi wa kutosha kuwa makundi makuu ya waasi katika jimbo la Darfur yanawatumia watoto, likiwemo lile lenye usemi mkubwa la Justice and Equality movement JEM. Serikali pia imewalazimisha watoto kujiunga na vikosi vyao kutokana na mapigano katika jimbo la Darfur ambayo yamewaathiri zaidi ya watu millioni 4.


Katika jamuhuri ya kidemocrasia ya Congo kufuatia hamasisho la mara kwa mara na shirika la UNICEF, kundi moja la wapiganaji limewaachilia huru watoto 195 waliokuwa wakitumikia kundi hilo kama wapiganaji.


Watoto hao waliokuwa katika kundi la MaiMai linaloipinga serikali, sasa wako mikononi mwa kitengo cha kuwalinda watoto cha jeshi la MONUC kinachoendesha shughuli zake kivu kaskazini. Hata hivyo shirika la umoja wa mataifa kuhusu watoto UNICEF linasema bado kuna karibu watoto elfu 2 wamesalia chini ya wapiganaji wa MaiMai.


Kwa mujibu wa shirika la UNICEF tatizo la kuingizwa watoto jeshini limekithiri katika bara la Afrika na Asia, japokuwa makundi ya watu waliojihami kutoka America na Mashariki ya kati yameripotiwa kuwatumia watoto.


Uasi wa zaidi ya miaka 18 wa kundi la Lords Resistance Army-LRA dhidi ya serikali nchini Uganda umelazimu zaidi ya Waganda millioni 1.6 nusu yao watoto kutoroka makwao na katika harakati hizo watoto hao wanajikuta mikononi mwa waasi hao.


Baadhi ya watoto wamelazimishwa kufanya uhalifu dhidi ya familia na jamii zao.Tangu kuanza kwa uasi na kundi la LRA nchini Uganda katika miaka ya 80 karibu watoto elfu 30 wametekwa nyara na waasi hao na kuingizwa jeshini.


Katika kuadhimisha siku hii ya leo ya kutumiwa watoto katika vikosi vya wanajeshi, hapa ujerumani katika mji wa Berlin rais Horst Koehler alipokea stakabadhi zilizotiwa saini kupinga hatua hiyo na stakabadhi nyingine kama hizo zilikabidhiwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bak-Ki Moon mjini NewYork Marekani.