default

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 18.10.2017 | 15:00

Raila aitisha maandamano ya nchi nzima 26 Oktoba

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ameitisha maandamano ya nchi nzima tarehe 26 mwezi Oktoba siku ambayo nchi hiyo inajiandaa kufanya uchaguzi mpya wa rais ambao ametangaza kuususia. Raila ameyasema hayo mbele ya maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wakimshangiria jijini Nairobi.Matamshi ya Odinga yamekuja katika wakati ambapo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi iebc Wafula Chibukati amewakosoa viongozi wa kisiasa pamoja na wafanyakazi wa tume hiyo saa chache baada ya kujiuzulu kwa kamishna mwadnamizi wa tume hiyo Roselyn Akombe aliyekimbilia nchini Marekani. Chebukati ameweka wazi kwamba hatokubali kuruhusu kuingiliwa tena kwa tume ya uchaguzi.Mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi ameongeza kusema kwamba viongozi wa kisiasa wanaotakiwa kuijenga nchi hiyo wamegeuka kuwa kitisho kikubwa kwa amani na uthabiti wa taifa.

Mgogoro kati ya Marekani na Uturuki bado kutatuliwa

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amesema nchi yake haiwezi kuyafuata matakwa ya Marekani wakati nchi hizo mbili zikifanya mazungumzo ya kujaribu kuutatua mvutano kuhusu suala la visa za usafiri.Mevlut Cavusoglu amelaani kile alichokiita mwelekeo usiokomaa wa kidiplomasia uliochukuliwa na Marekani na kukosoa athari za mzozo usiokuwa na haja dhidi ya raia wa Kituruki. Amesema Uturuki iliunga mkono ushirikiano na Marekani lakini akasisitiza kwamba vyombo vya sheria nchini humo viko huru.Ujumbe wa Marekani uliwasili Jumatatu mjini Ankara kwa ajili ya mazungumzo yaliyolenga kuutatua mvutano baina ya nchi hizo mbili.Marekani ilisimamisha huduma nyingi za utoaji visa kwa raia wa Uturuki katika ofisi zake za ubalozi nchini Uturuki, na Uturuki ikachukua hatua kama hiyo kulipiza kisasi kwa kusimamisha huduma ya utoaji visa katika balozi zake nchini Marekani kwa raia wa Marekani.

Mfalme wa Qatar atowa mwito wa kuondolewa vikwazo na jirani zake wanaovutana.

Mfalme wa Qatar amezitolea mwito nchi jirani kuondowa vikwazo vya kibiashara alivyovitaja kuwa visivyo vya haki vilivyodumu miezi minne dhidi ya nchi yake akisema yuko tayari kuanzisha mazungumzo ya kuumaliza mgogoro huo wa kidiplomasia. Mfalme Tamim bin Hamad Al-Thani aliyewasili Jumanne nchini Indonesia akitokea katika ziara ya kiserikali nchini Malaysia amesema katika mkutano na waandishi habari wa pamoja na rais wa Indonesena Joko Widodo, kwamba mvutano huo unaziathiri nchi zote zinazohusika. Saudi Arabia,Bahrain,Misri na Umoja wa Falme za kiarabu zilikata uhusiano na Qatar Juni 5 mwaka huu kufuatia madai kwamba nchi hiyo inaunga mikono makundi ya itikadi kali katika kanda hiyo na ina uhusiano wa karibu zaidi na Iran ambayo ni hasimu wa nchi hizo.

Duru ya mwanzo ya mazungumzo ya kuunda serikali yakamilika ujerumani

Muungano wa kihafidhina wa Kansela Angela Merkel umemaliza duru ya kwanza ya mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya mseto.Maafisa wa vyama hivyo wamesema kwamba mazungumzo hayo yaliyochukua muda wa masaa mawili yalikuwa na tija. Peter Tauber katibu mkuu wa chama cha Knasela Angela Merkel cha Christian Demokratic Union CDU amesema mazungumzo yalikuwa ya maana yakihusisha kubadilishana hoja.Kauli hiyo imekuja baada ya duru ya mwanzo kati ya chama cha CDU,na chama ndugu cha Bavaria CSU pamoja na chama kinachoelemea biashara cha Free Demorats FDP. Kauli ya Tauber imeonesha kuunga mkono kilichosemwa na FDP na CSU kuhusu mazungumzo hayo. Katibu mkuu huyo wa chama cha CDU amesema chama chake kinahisi kuna dalili nzuri kuhusu mkutano mwingine utakaofanyika pamoja na walinzi wa mazingira Die Grune baadae leo, chama ambacho pia kimo katika majadiliano ya kuunda serikali mpya ya mseto.

Sheria tata ya kupambana na ugaidi yapitishwa Ufaransa

Bunge la Ufaransa limeipitisha sheria mpya yenye utata ya kupambana na ugaidi. Sheria hiyo iliyopewa msukumo na rais Emmanuel Macron na kukosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu inawapa maafisa madaraka ya kudumu ya kufanya msako ndani ya majumba ya watu, kuzifunga sehemu za ibada na kudhibiti uhuru wa kutembea.Kura hiyo ya mwisho juu ya muswaada huo wa sheria imepitishwa na baraza la seneti baada ya wabunge wa bunge la kitaifa kuipitisha kwa wingi mnamo wiki iliyopita.Sheria mpya ya kupambana na ugaidi imeundwa kwa lengo la kumaliza sheria ya hali ya dharura ya miaka miwili nchini Ufaransa iliyowekwa tangu yalipotokea mashambulizi ya kigaidi mnamo Novemba mwaka 2015.Kura hiyo ya leo inakuja wakati ambapo rais Macron anasubiriwa kutowa hotuba yake muhimu juu ya usalama ambapo anatarajiwa kutangaza mipango yake ya kuongeza bajeti kwa ajili ya polisi na mashirika ya kijasusi.

Kiongozi wa juu wa Iran amjibu Trump

Kiongozi wa juu nchini Iran Ayatollah Khamenei amepuuza ukosoaji unaotolewa na rais wa Marekani Donald Trump.Katika hotuba yake aliyoitowa leo Khamenei ameutaja ukosoaji huo kama ni kelele na kauli zisizokuwa na uhalisia zinatolewa na mtu katili. Akiwahutubia wanafunzi mjini Tehran kiongozi huyo wa juu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hawezi kupoteza muda kumjibu rais huyo wa Marekani.Kauli ya Khamenei ni ya kwanza ya kiongozi huyo ikimjibu Trump baada ya hotuba yake ya ijumaa iliyopita ambapo alitaka paweko vikwazo vikali vitakavyoizuia Iran katika kile alichokiita shughuli zake za kuvuruga usalama katika Masharii ya Kati.

Mkutano wa kilele kuhusu maziwa makuu kuijadili mizozo kadhaa ya eneo hilo

Migogoro inayoendelea kuzikumba nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Burundi na Sudan Kusini, inatarajiwa kuugubika mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa 12 mjini Brazzaville kesho Alhamisi. Mkutano huo utawaleta pamoja viongozi wakuu wa serikali kutoka Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, DRC, Jamhuri ya Congo, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Maafisa wa usalama, wakuu wa majeshi na mawaziri wa mambo ya nje walifanya mikutano ya awali siku za Jumapili na Jumatatu katika mji mkuu wa Jamhuri ya Congo - Brazzaville. Kundi hilo la mataifa linafahamika kwama Mkutano wa Kimataifa kuhusu kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR), na walikutana mara ya mwisho Juni 2016.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com

Albanian Shqip

Amharic አማርኛ

Arabic العربية

Bengali বাংলা

Bosnian B/H/S

Bulgarian Български

Chinese (Simplified) 简

Chinese (Traditional) 繁

Croatian Hrvatski

Dari دری

English English

French Français

German Deutsch

Greek Ελληνικά

Hausa Hausa

Hindi हिन्दी

Indonesian Bahasa Indonesia

Kiswahili Kiswahili

Macedonian Македонски

Pashto پښتو

Persian فارسی

Polish Polski

Portuguese Português para África

Portuguese Português do Brasil

Romanian Română

Russian Русский

Serbian Српски/Srpski

Spanish Español

Turkish Türkçe

Ukrainian Українська

Urdu اردو