1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ILULISSAT: Merkel aendelea na ziara yake Greenland

17 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBYJ

Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, na waziri wa mazingira, Sigmar Gabriel, wamo nchini Greenland kwa ziara rasmi ya siku mbili.

Viongozi hao wamejionea athari zilizosababishwa na ongezeko la joto duniani wakati walipotembezwa eneo la magharibi mwa Greenland kwa njia ya helikopta.

Wanasayansi walio nchini Greenland, kisiwa kikubwa duniani, kinachojitawala lakini kilicho chini ya ufalme wa Danemark, walikuwa na jukumu la kumuonyesha kansela Merkel uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo hilo.

Kansela Merkel amesema atatumia urais wa Umoja wa Ulaya kushinikiza mkutano kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda duniani na nchi kubwa zinazoendelea kama vile China na India, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mkutano wa mawaziri wa mazingira unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa nchini Bali mwezi Disemba mwaka huu.

Kiongozi huyo pia anatarajiwa kuhutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza tarehe 25 mwezi ujao na kuhuduria mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa mjini New York Marekani ulioitishwa na rais wa Marekani, George W Bush.