1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imam Ghazi auwawa

Oummilkheir10 Julai 2007

Mapigano makali yaliyogharimu maisha ya watu dazeni kadhaa, yanaendelea katika msikiti mwekundu,huku ripoti za kuaminika zikizungumzia juu ya kuuliwa Immam Ghazi ,alipotaka kujisalimisha kwa vikosi vya serikali.

https://p.dw.com/p/CB2v
Kiongozi wa waasi wa msikiti mwekundu Abdul Rashid Ghazi
Kiongozi wa waasi wa msikiti mwekundu Abdul Rashid GhaziPicha: AP

Vikosi vya usalama vya Pakistan vimemuuwa mkuu wa waazi Abdul Rashid Ghazi,vilipokua vilipouvamia msikiti mwekundu mjini Islamabad.Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ameliambia shirika la habari la Reuters Ghazi ameuliwa katika awamu ya mwisho ya mapigano.Jawad Cheema ameendelea kusema Abdul Rashid Ghazi alikua amefuatana na wanamgambo wanne au watano na alikua tayari kusalim amri alipopigwa risasi na waasi wenzake.

Mapigano yaliyoanza alfajiri ya leo yameshagharimu maisha ya watu wasiopungua 60 hadi sasa.

Na idadi hiyo inahofiwa huenda kuongezeka. ”Maiti zimetapakaa kila mahala” amesema bwana mmoja aliyejificha msikitini,alipohojiwa kwa simu na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Miripuko mikubwa na milio ya risasi imekua ikisikika na moshi kutapakaa kutoka jengo hilo kubwa lenye msiskiti na madrasa.Inahofiwa pengine moshi huo unatoka ndani ya chuo cha Qoraani cha wasichana.Magari ya kuwasafirisha wagonjwa yanakwenda na kurudi na honi kuhanikiza mjini Islamabad.Na familia za waliofungiwa ndani ya jengo hilo zimejazana nje na kuhanikiza kwa vilio.

“Wafuasi wa itikadi kali wanajibu mashambulio kwa kufyetua risasi za rashasha,mabomu ya mkono na makombora-“ amesema hayo msemaji wa jeshi jenerali Waheed Arshad kupitia televisheni ya taifa.

Wanamgambo 50 wamesalim amri milio ya risasi iliposita kidogo.

Msemaji huyo wa jeshi ameongeza kusema vikosi vya serikali vimekomboa asili mia 80 ya jengo hilo.

“Wanawake na watoto wako katika sehemu ya chini ,alikokua amejificha hapo awali Abdul Rashid Ghazi”.

Wanawake kama sitini hivi na watoto wameshatolewa lakini,kwa mujibu wa maafisa wa serikali wanamgambo kama mia moja hivi wanaoongozwa na wafuasi wa al Qaida wanaudhibiti msikiti huo na kuwashikilia kama ngao wanafunzi kati ya mia tatu na mia nne,wakiwemo pia wanawake na watoto.

“Nataraji tutaweza kuwaokoa watu wengi zaidi” amesema waziri wa mambo ya ndani Aftab Sherpao aliyemtupia Imam Abdul Rashid Ghazi dhamana ya yanayotokea.Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Jazeed Iqbal Cheema anasema: “Kulikua na dalili nzuri na tulitaraji pengine makubaliano yangepatikana,lakini kwa bahati mbaya Ghazi alibadilisha msimamo wake wa awali na kusababisha mazungumzo kuvunjika.”

“Jeshi linajitahidi kuepusha hasara” amesema jenerali Arshad aliyeongeza kusema vikosi vya usalama vinapekua kila chumba kati ya 75 vya jengo hilo.

Umoja wa ulaya umeelezea masikito yake kutokana na hasara ya maisha na kutoa mwito mazungumzo yaendelezwe kati ya serikali na wanamgambo.

Nayo Finland imeamua kuufunga kwa muda ubalozi wake mjini Islamabad.Ubalozi huo unakutikana karibu na jengo la msikiti mwekundu.