1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imeshindikana kulinda wanyamapori?

Mohammed Khelef
27 Septemba 2016

Kongamano la biashara ya viungo vya wanyamapori na hifadhi ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka linaendelea Johannesburg. Nchi 20 za Kiafrika na Marekani zinataka masoko ya pembe za ndovu yafungwe kabisa.

https://p.dw.com/p/2Qcr6
Artikelbild Südafrika
Picha: Jürgen Schneider

Bado mdahalo ni mkubwa kwenye Kongamano la Kupambana na Biashara Haramu ya Viumbe Vilivyo Hatarini, CITES, ambalo linawaleta pamoja wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 180 duniani. Kongamano hili lililofunguliwa Jumamosi litaendelea kwa wiki mbili nzima, likiangazia mabadiliko kwenye udhibiti wa biashara ya kiasi cha viumbe 500, lengo likiwa kuthibiti biashara haramu na kuimarisha uendelevu wa biashara halali.

Biashara ya kimataifa ya pembe za ndovu ilipigw amarufuku tangu mwaka 1990, lakini marufuku hiyo haihusiani na masoko ya ndani, ingawa yako mataifa kadhaa - kama vile Kenya na Marekani - ambayo tayari yamepiga marufuku. Kisheria, pembe za ndovu zinazouzwa ndani ya nchi ni lazima ziwe zimepatikana kisheria, lakini kiwango cha udhibiti hakitoshi, anasema Peter LaFontaine kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Ustawi wa Wanyama, IFAW.

EU yapinga marufuku ya kuuza pembe za ndovu

Pembe za ndovu zilizokamatwa Kenya zachomwa moto
Pembe za ndovu zilizokamatwa Kenya zachomwa motoPicha: Getty Images/AFP/C. de Souza

"Biashara ya ndani ya pembe za ndovu huwa inatumika kama upenyo kwa wauzaji wa kimataifa kuutumia kama njia ya kutakatisha kile kinachopatikana kwa njia haramu," anasema Satyen Sinha, mshauri kwenye shirika hilo la IFAW. Ni kwa mantiki hiyo, ndipo sasa wapiga kampeni wanaamini kuwa kuyafungia masoko ya ndani kutakuwa na maana kubwa ya kwenye masoko ya kimataifa, katika wakati huu ambapo idadi ya tembo inashuka kwa kasi sana barani Afrika.

Ni jambo la kushangaza kuwa Umoja wa Ulaya haukubaliani na marufuku hiyo, ukisema unataka kuona biashara ya ndani ikiendelea, hasa kwa vitu vinavyotokana na pembe za ndovu. "Tunakubali kuwa soko la ndani lazima liangaziwe, lakini ikiwa tu lina mafungamano na soko la kimataifa," anasema Gael de Rotalier, mkuu wa timu ya Umoja wa Ulaya kwenye kongamano hilo.

Lakini si tembo pekee walio kwenye kitisho cha kutoweka duniani kutokana na biashara haramu ya viungo vyao. Ndege aina ya kwembe, ambaye mdomo wake mkubwa huchukuliwa na majangili kuwa una madini yale yale yanayopatikana kwenye pembe ya ndovu, nao sasa wako hatarini.

Ndege wako hatarini pia

Ndege aina ya kwembe huuliwa na majangili
Ndege aina ya kwembe huuliwa na majangiliPicha: Getty Images/AFP/R. Gacad

Ndege hao, ambao wengine huwaita "mbawa za ndovu" ni sehemu ya viumbe wanaouawa na midomo yao kupelekwa China kwenye soko kubwa la kusini mwa Asia. Mkutano huu wa kuwalinda viumbe, unahusu pia ndege hawa. "Kampeni kubwa ya kimataifa ya kupambana na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu, inapata mafanikio, lakini sasa kwa gharama ya kuangamizwa kwembe," anasema Richard Thomas wa mradi wa TRAFFIC ulio na makao yake nchini Uingereza.

Uwindaji wa kwembe ulianza kushamiri mwaka 2010, hasa nchini Indonesia. Inasemwa kuwa muda huo pia ndipo kiwango cha uwindaji tembo kilipokuwa juu, na hivyo kampeni dhidi ya uwindaji huo, bali pia na kushuka kwa idadi ya tembo, vikawa vichocheo vya kuwageukia kwembe. Kufikia mwaka jana, kwembe akawa amewekwa kwenye Mkataba wa CITES kuwa miongoni mwa viumbe walio hatarini zaidi kutoweka.

Kwenye mataifa mengi ya kusini mwa Asia, ndege huyu anayeishi kwenye maeneo ya karibu na vianzio vya maji ni alama ya uhai na umauti. Mabawa yake yamekuwa yakitumiwa kwenye sherehe za kijadi, kwani wakati wa uzazi, kwembe mke hunyonyolewa mabawa yote na kukaa ndani akilalia na kumtegemea mume pekee kulisha familia.

Kinachowaponza kufikiwa haraka na majangili ni kuishi kwao kwenye magogo mabovu, majengo ya kale na pia sauti yao nzito ambayo ni rahisi kuwasikia walipo, hata mtu anapokuwa mbali, anasema Thomas wa shiika la TRAFFIC.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP
Mhariri: Saumu Yussuf