1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yaadhimisha miaka 60 ya uhuru

Josephat Charo15 Agosti 2007

India leo imeadhimisha miaka 60 ya uhuru kutoka kwa Uingereza, huku mgomo katika jimbo la Kashmir, ukikwamisha shughuli za kibiashara.

https://p.dw.com/p/CH9Y
Waziri mkuu wa India Manmohan Singh
Waziri mkuu wa India Manmohan SinghPicha: AP

Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh ameadhimisha miaka 60 ya uhuru wa India kutoka kwa ukoloni wa Uingereza kwa kuwataka raia wafanye kazi kwa bidii kuondokana na umaskini, ujinga na magonjwa. India haipaswi kuwa nchi yenye visiwa vilivyoendelea sana na huku maeneo mengine yakiwa bado yameachwa nyuma katika maendeleo na ambako watu wachache wananufaika kutokana na faida za maendeleo.

´Tumesonga mbele katika vita dhidi ya umaskini, ujinga na magonjwa. Lakini je tunaweza kusema tumevishinda vita hivyo? Ameuliza waziri mkuu Manmohan Singh wakati alipokuwa akiwahutubia maafisa na wanadiplomasia pamoja na watoto waliokuwa wamevaa mavazi ya rangi nyeupe, manjano na kijani kibichi, rangi za bendera ya India, kwenye ngome nyekundu ya kihistoria mjini New Delhi.

Maafisa wa usalama walio stadi kwa kufyatua risasi walishika doria katika majumba yaliyo karibu na mahala alipokuwa akihutubia waziri mkuu Manmohan Singh, huku vikosi vya jeshi na maafisa wa polisi waliojihami na silaha wakilinda barabara na majengo muhimu kwenye sehemu mbalimbali za India katika siku ambayo kitamaduni hugubikwa na mashambulio ya wanamgambo waliojitenga au waasi wa Mao.

Hapo awali waziri mkuu Manmohan Singh aliweka mashada ya maua kumkumbuka kiongozi wa vuguvugu la uhuru nchini India, Mahtma Gandhi, waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, Jawaharlal Nehru na msichana wake, waziri mkuu wa zamani aliyeuwawa, Indira Gandhi.

Katiba hotuba yake iliyoonyeshwa kwenye televisheni, rais wa India, Pratiba Patil, alimetoa mwito maendeleo ya kiuchumi nchini India yaweze kuwanufaisha raia wote.

´Matunda ya maendeleo ya kiuchumi sharti yaweze kuboresha hali za kimaisha na kazi za wananchi wetu wanaofanya kazi kwa bidii na watu ambao bado wanaishi katika hali ngumu ya umaskini.´

Rais Patil pia amewapongeza wanawake wa India kwa juhudi zao katika maendeleo.

´Historia inadhihirisha kwamba wanawake wetu wamejiendeleza sio tu kama wajenzi wa familia lakini pia wamejitolea kwa dhati kuijenga nchi.´

Sambamba na sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya uhuru, mgomo ulioongozwa na waasi umekwamisha shughuli za kila siku katika jimbo la Kashmir. Duru za polisi zinasema maafisa wa usalama wamepelekwa katika eneo hilo kukabiliana na mashambulio ya waasi.

Mgomo huo uliodhaminiwa na muungano wa kisiasa wa waasi, uliwalazimu watu wazikimbie barabara za mji mkuu wa Kashmir, Srinagar, huku wenye maduka na wafanyabiashara wakilazimika kuyafunga maduka yao na maeneo ya biashara. Hali hiyo pia ilitanda katika miji mingi iliyo na idadi kubwa ya waislamu lakini hali ilikuwa shwari mjini Jammu, mji ulio na idadi kubwa ya Wahindi.

Wanamgambo wa Kashmir na waasi huitazama siku ya uhuru wa kitaifa kuwa yenye bahati mbaya. Kiongozi wa waasi, Syed Ali Geelani amesema mgomo wa leo unalenga kuuambia ulimwengu kwamba Kashmir inataka kuwa na haki ya kujitawala.