1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yajiandaa kwa uchaguzi mkuu

14 Aprili 2009

Wadadisi waashiria kutaundwa serikali nyengine ya muungano

https://p.dw.com/p/HVlQ
Waziri mkuu Manmohan Singh.Picha: AP

India inajiandaa kwa uchaguzi mkuu kuanzia Alhamisi ijayo tarehe 16 mwezi huu wa Aprili hadi tarehe 13 Mei, katika zoezi kubwa kabisa la demokrasia duniani. Chama tawala cha CONGRESS cha waziri mkuu Manmohan Singh kinakabiliwa na upinzani mkali kutoka chama kikuu cha upinzani BHARATIYA JANATA.

Katika bunge la sasa Congress kina viti vingi zaidi na wadadisi wanashiria huenda kikarudia tena matokeo ya uchaguzi wa miaka mitano iliopita na kuibuka mshindi.

Chama cha Congress cha waziri mkuu Manmohan Singh kinaongoza hata hivyo serikali ya muungano ya ule ushirika unaojulikana kama United Progressive Alliance-UPA- ulioanzishwa mwaka jana na chama hicho katika jimbo moja nchini humo baada ya kukosa uungaji mkono wa washirika wao wa mrengo wa shoto, kutokana na mzozo juu ya makubaliano yaliofikiwa na Marekani kuhusu nuklea kwa matumizi ya kiraia.

Wakati mwanauchumi mpole Manmohan Singh ni waziri mkuu, hata hivyo wengi wanasema nguvu za madaraka zimo mikononi mwa kinara wa chama anayetokana na ukoo wa Nehru na Ghandi, Bibi Sonia Ghandi.

Bibi Ghandi na mwanawe wa kiume Rahul, wanaangaliwa kuwa nguzo mbili muhimu za chama cha Congress.

Chama kikuu cha upinzani BHARATIYA JANATA-BJP, nacho pia kinauongoza ushirika wa vyama unaojulikana kama National Democratic Alliance-NDA-

BJP kina sifa za kuwa na sera inayopendelea masoko, lakini kilipoteza madaraka katika uchaguzi mkuu wa 2004 kutokana na kile wengi wanachoamini ulikua ukosefu wa kuona mbali kuhusiana na kauli yake mbiu " India inayongara," kwani licha ya ukuaji wa kiuzchumi, kauli mbiu hiyo ilishindwa kuendana na ukweli wa hali halisi na hivyo mamilioni ya masikini kuachwa nyuma na mafanikio hayo ya kiuchumi katika taifa hilo la tatu kwa ukubwa wa kiuchumi barani Asia.

L.K. Advani
Kiongozi wa Baratiya Janata, L-K.Advani.Picha: UNI

Kiongozi wa BJP L-K.Advani mwenye umri wa miaka 81 anatajwa kuwa ni mwanasiasa mkakamavu na mzungumzaji mzuri, lakini wengine wanahisi umri wake hautokua kivutio kwa wapiga kura vijana ambao idadi yao imeongezeka katika uchaguzi huu. BJP kimekosolewa vikali siku za nyuma ikidaiwa kimechochea mivutano na hali ya wasi wasi baina ya Wahindu na waislamu walio wachache katika taifa hilo ambalo kikatiba ni la watu wa dini mbali mbali.

Pia kuna chama cha Kikoministi. Hiki ni chama kikubwa cha mrengo wa shoto kilichokisaidia kile cha Congress kuingia madarakani miaka mitano iliopita na hata kukiunga mkono kwa miaka minne kabla ya kujitenga mwaka jana kikipinga mkataba wa nuklea kati ya India na Marekani. lakini tangu wakati huo kimejongeleana na mshirika wake wa zamani kikisema kinaweza kuzingatia kukiunga mkono tena chama cha Congress na uwezekano wa kuunda serikali ijayo.

Wakoministi wana tawala katika majimbo matatu, likiwemo lile lenye wakaazi wengi la West Bengal na wapinzani wamekilaumu kwa kuzorotesha mageuzi ya kiuchumi, wakati kilipogawana madaraka na Congress. Chama hicho cha kikoministi kina shaka shaka na hatua ya kuwa na ushirikiano wa karibu na Marekani.

Vyama vyengine ni SAMAJWADI . Hiki kinaongozwa na mchezaji mieleka wa zamani mwenye historia ndefu ya makosa ya jinai na kimewavutia baadhi ya wachezaji senema nyota nchini India.

Ama BAHUJAN SAMAJ-BSP- kinachotawala katika jimbo la Ultra Pradesh lenye idadi kubwa kabisa ya wakaazi nchini India,kinaungwa mkono zaidi na watu wa tabaka la masikini wanaojulikana kama " wasioguswa." Chama hiki kinaangaliwa kama nguzo muhimu miongoni mwa vyama vidogo vidogo, pindi serikali ya muungano itahitajika.

kwa jumla wachambuzi wanasema yeyote atakayeshinda uchaguzi huo mkuu nchini India hatoweza kuibuka na wingi wa kutosha bungeni kuunda serikali peke yake na hivyo serikali ya mseto itahitajika.

Mwandishi Abdul-Rahman RTRE

Mhariri Saumu Mwasimba