1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Indonesia na Malaysia kuruhusu wakimbizi kuingia nchini mwao

20 Mei 2015

Malaysia na Indonesia zimekubali kuwaruhusu maelfu ya wahamiaji wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar na wale kutoka Bangladesh kuingia katika nchi hizo. Wakimbizi hao wamekwama baharini kwa siku kadhaa sasa.

https://p.dw.com/p/1FT38
Picha: Reuters/Stringer

Waziri wa mambo ya nje wa Malaysia Anifah Amas amesema nchi yake na Indonesia zimekubaliana kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa wahamiaji haramu 7,000 ambao bado wamekwama baharini na kuwapa makaazi ya muda, huku mchakato wa kuwapa makaazi na kuwarejesha makwao ukishughulikiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao na jumuiya ya kimataifa.

Anifah ameonya kuwa Malaysia na Indonesia hazina raslimali za kutosha kuwasaidia wahamiaji hao na kuutaka ulimwengu kushirikiana nao kuwasaidia wahamiaji hao na kuongeza kuwa nchi hizo mbili hazitajishughulisha katika kuwatafuta na kuwaokoa wahamiaji hao baharini bali zitawasaidia tu wale watakaofika katika fukwe zao.

Myanmar pia imelegeza sera

Myanmar kwa upande wake imeonekana kulegeza sera zake zinazochukuliwa za kibaguzi dhidi ya watu wa jamii ya Rohingya kwa kusema iko tayari pia kuwasaidia wahamiaji hao huku shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa zikizidi kutaka wahamiaji hao kupokea misaada kutoka kwa Thailand, Malaysia na Indonesia.

Wahamiaji wa Rohingya wakikata kiu wakisubiri hifadhi Indonesia
Wahamiaji wa Rohingya wakikata kiu wakisubiri hifadhi IndonesiaPicha: Reuters/Beawiharta

Myanmar imesema inatiwa wasiwasi na hali ya wahamiaji hao wanaohangaika baharini na inafuatilia kwa karibu matukio hayo. Wengi wa wahamiaji hao waliokwana ni wa kutoka jamii ya Rohingya ambao hawatambuliki rasmi na serikali ya Myanmar wanaowachukulika wahamiaji kutoka bengali, huku wakidharauliwa pakubwa na makundi mengine nchini humo.

Nchi husika kufanya mkutano

Mawaziri wa mambo ya nje wa Thailand, Malaysia na Indonesia wanatarajiwa kukutana hii leo mjini Kuala Lumpur kujadili tatizo hilo la kukwama kwa wahamiaji hao baharini ambao hakuna taifa linaloridhia kuwahifadhi. Myanmar hata hivyo imeususia mkutano huo kwa kusema haingependa kulifanya suala hilo kuwa la kimataifa.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Thailand, Malaysia na Indonesia
Mawaziri wa mambo ya nje wa Thailand, Malaysia na IndonesiaPicha: picture-alliance/dpa/F. Ismail

Wakati huo huo, wavuvi nchini Indonesia wamewaokoa wahamiaji 370 hii leo waliokuwa wamekwama kwa boti mbili katika jimbo la Aceh. Mkuu wa shirika la uokozi la mji wa Langsa Khairul Nova amesema wahamiaji hao kutoka jamii ya Rohingya walikuwa wameishiwa maji mwilini, wana njaa na wamedhoofika mno.

Uokozi huo unakuja siku moja tu baada ya jeshi la Indonesia kuwataka wavuvi kutowasaidia wahamiaji waliokwama majini. Idadi ya wahamiaji waliokolewa katika jimbo hilo la Aceh mwezi huu imefikia 1,800. Shirika la umoja wa mataifa la kushughulikia wakimbizi UNHCR linakadiria kiasi ya wahamiaji 2,000 huenda bado wamekwama majini kati ya Myanmar na Bangladesh.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/Afp

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman