1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Infantino anakabiliwa na changamoto kubwa

27 Februari 2016

Rais mpya wa FIFA Gianni Infantino anakabiliwa na jukumu kubwa la kuleta mabadiliko na kuliunganisha kandanda la ulimwengu

https://p.dw.com/p/1I3Nt
Schweiz Neuer FIFA Präsident Gianni Infantino
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Hayo ni wakati rundiko la migogoro inayotokana na enzi ya Sepp Blatter iliyogubikwa na kashfa likihitaji kuchukuliwa hatua ya haraka.

Infantino, afisa mkuu katika shirikisho la kandanda la Ulaya – UEFA, ameahidi kuweka kikomo kwa siku za giza katika FIFA baada ya ushindi wake wa kishindo katika uchaguzi. Lakini raia huyo Mswisi mwenye asili ya Kiitaliano tayari anakabiliwa na changamoto chungu nzima. Wachezaji mahiri kabisa wa kandanda pamoja na washirika wakuu wa ufadhili lazima washawishike kuwa FIFA inaweza kuirekebesha nyumba yake. "ningependa kuzungumza na wadau, na mashirikisho ya kitaifa, na ligi mbalimbali, vilabu, wachezaji, na mashabiki na nataka kuwaambia nyinyi nyote; mtajivunia FIFA, mtajivunia kile FIFA itaufanyia mchezo wa kandanda. Sasa tunaingia katika enzi mpya. Umekuwa mkutano muhimu ambapo baadhi ya mageuzi yameidhinishwa, baadhi yamekuwa mageuzi ya kihistoria, ambapo rais mpya amechaguliwa na atayatekeleza mageuzi haya yote ili kuhakikisha kuwa taswira na hadhi ya FIFA vonarejeshwa tena".

Schweiz Zürich FIFA Außerordentlicher Kongress Stimmenzahl
Infantino alishinda urais wa FIFA katika duru ya pili ya uchaguzi na kumpiku Sheikh Salman wa BahrainPicha: Reuters/R. Sprich

Infantino pia atastahili kuyapa kipau mbele maslahi ya kuyaimarisha mataifa ya kandanda barani Asia na Afrika, mabara mawili ambayo yalimuunga mkono hadharani Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa wa Bahrain aliyemaliza katika nafasi ya pili kwa matumaini kuwa kiongozi asiyetoka Ulaya angeongoza FIFA baada ya urais wa miaka 18 ya rais wa Uswisi Blatter.

Infantino anasema mageuzi ya utawala yaliyopitishwa saa chache kabla ya kuchaguliwa kwake yalikuwa “ya kihistoria” na kuwa kuyatekeleza ndio jambo la kipaumbele.

Mageuzi hayo ni pamoja na mabadiliko ya usimamizi wa FIFA, kuyapunguza mamlaka ya Infantino ikilinganishwa na nguvu alizokuwa nazo Blatter.

Patakuwa na ukomo wa muhula wa miaka 12 kwa maafisa wakuu na mishahara yao itafichuliwa. Kamati kuu yenye mamlaka makubwa sasa itaitwa baraza la FIFA, na shughuli za kibiashara za thamani ya mabilioni ya dola zitaendeshwa tofauti na siasa za kandanda.

Lakini hakukuwa na uamuzi wa kuundwa jopo la nje ambalo limekuwa likipigiwa upatu kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro wa rushwa katika FIFA. Wafadhili wakuu wa Kombe la Dunia walisema baada ya uchaguzi huo wa jana kuwa “uchunguzi huru wa mageuzi hayo” bado tu ndio mkakati bora wa kuhakikisha mabadiliko ya kweli.

Blatter, aliyepigwa marufuku kujihusisha na mausala ya kandanda kwa miaka sita kuhusuana na ukiukaji wa maadili, amempongeza Infantino lakini alimwachia mrithi huyo kazi ngumu ya kufanya.

Wakati huo huo, shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA litaamua katika mkutano wa kamati kuu wa Machi 4, nani atakayekuwa Katibu Mkuu wake baada ya Gianni Infantino kuchaguliwa kuwa rais wa FIFA.

Kwa mujibu wa sheria za UEFA, Infantino lazima ajizulu wadhifa wake maramoja wa katibu mkuu. Naibu wake Theodore Theodoridis wa Ugiriki huenda akachaguliwa kuwa mrithi wake katika mkutano huo wa Ijumaa wiki ijayo. Infantino alikuwa katibu mkuu w UEFA tangu 2009, na alifanya kazi katika shirikisho hilo tangu 2000.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamedn Dahman