1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IOC yakanusha ilificha vipimo vya wanamichezo

Bruce Amani
3 Aprili 2017

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC imekanusha leo kuwa ilificha matukio ya matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu miongoni mwa wanamichezo katika mashindano ya Olimpiki ya 2008 mjini Beijing

https://p.dw.com/p/2aacl
IOC-Präsident Thomas Bach
Picha: picture alliance/dpa/Y. Hyung-Jae/Yonhap/AP

Hii ni baada ya kipindi cha televisheni ya Ujerumani kufichua kuwa vipimo vilivyoonyesha kuwa wanaridha wa Jamaica walitumia dawa hizo hayakushughulikiwa. Makala hiyo ilisema wanamichezo kadhaa wa Jamaica walikuwa na dalili za clenbuterol, kirutubisho cha kujenga misuli kilichopigwa marufuku, katika vipimo vya karibuni vilivyofanywa upya kwenye sampuli za mkojo ziliodumu miaka minane. Hakuna wanamichezo waliotajwa majina yao. IOC imesema hakuna dalili zozote za udanganyifu wa kupangwa, baada ya kushauriana na Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Dawa zilizopigwa marufuku michezoni - WADA.

Hivyo basi IOC imesema katika taarifa kuwa haitafuatilia tena kesi hizo. Iliongeza kuwa viwango vidogo vya virutubisho vya clenbuterol vilivyopatikana kwenye sampuli za mkono vinaashiria matukio ya uwezekano wa kuchafuliwa nyama walizokula wanariadha. China inatumia sana dawa hizo kwa kuwapa mifugo wake na wanamichezo walipewa onyo kabla ya kwenda Beijing

IAAF yadukuliwa na Urusi

Katika taarifa nyingine inayohusiana na riadha ni kuwa Shirikisho la Kimataifa la Riadha – IAAF limesema limekumbwa na udukuzi wa mtandaoni unaoshukiwa kufanywa na Urusi ambao linaamini umehujumu habari kuhusu taarifa za matibabu ya wanamichezo.

Katika taarifa, IAAF imesema kikundi cha udukuzi cha Urusi kinachofahamika kama Fancy Bears kinaaminika kufanya shambulizi hilo la mtandao mwezi Februari na kuwa lilizilenga habari zinazohusu maombi ya wanamichezo kuhusu aina ya dawa wanazoweza kutumia kutokana na maradhi mbalimbali. Shirikisho hilo limesema limewasiliana na wanamichezo waliotuma maombi yao ya matibabu hayo tangu mwaka wa 2012 na rais wake Sebastian Coe ameomba radhi. Kikundi cha Fancy Bear bado hakijaizungumzia suala hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga