1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Irak kweli itaweza kudhibiti hali?

Maja Dreyer3 Septemba 2007

Tuanze na zile habari za kutoka Iraq zinazosema kuwa Waingereza wanataka kuondoka mjini Basra na kukabidhi mamlaka kwa wanajeshi wa Iraq.

https://p.dw.com/p/CHRx
Kutoka magazeti ya humu nchini
Kutoka magazeti ya humu nchiniPicha: dpa

Wahariri wa magazeti ya humu nchini wana wasiwasi juu ya mkakati huo wa Uingereza, kama tunavyosoma katika gazeti la “Müncher Merkur”:

“Hakuna ishara yoyote inayoleta matumaini kwamba serikali ya Iraq itaweza kuhakikisha usalama hivi punde. Vipi tena ingeweza kudhibiti hali bila ya wananchi kuiunga mkono na bila ya msaada kutoka nje? Mtu anayeamini kuwa hali haiwezi kuwa mbaya zaidi ataona kwamba hiyo si kweli, pindi majeshi ya kigeni yatakapoondoka katika nchi hiyo ya vita.”

Na zaidi juu ya suala hili hili ameandika mhariri wa “Braunschweiger Zeitung”:

“Inaonekana kama jeshi la Uingereza na waziri mkuu mpya Gordon Brown wako tayari kumaliza ujumbe wake nchini Iraq na kujiondoa kutoka mji wa Basra. Lakini kwa kusema kuwa Wairaki wenyewe wanaweza kuhakikisha usalama, mzozo ndani ya nchi hiyo utakuwa kama ule wa Vietnam. Tena tayari mamia ya watu, wakiwa ni raia wa kawaida au wanajeshi wameshauawa. Suali la msingi lakini, yaani vipi jumuiya ya kimataifa iwashughulikie madikteta, bado halijatatuliwa.”

Ni uchambuzi wa mhariri wa “Braunschweiger Zeitung” juu ya uamuzi wa Uingereza kukabithi mamlaka ya eneo la Basra kwa Wairaki na kujiondoa.

Mada ya pili ni kuchapishwa kwa kibonzo cha kumkabehe mtume Mohammed katika gazeti moja la Sweden ambacho kimezusha upinzani katika nchi kadhaa za Kiarabu. Ndiyo sababu mhariri wa “Kölnische Rundschau” anauliza:

“Je, hamjajifunza chochote? Baada ya kuchapishwa kwa vibonzo vya kumkashifu mtume Mohammed nchini Denmark mwaka mmoja na nusu uliopita na watu wasiopungua 100 waliuawa katika maandamano na mapigano yaliyozuka, bado gazeti la Sweden limechapisha kibonzo cha aina hiyo likidai kuwa ni uhuru wake kutoa maoni yake. Bila shaka, haki hiyo ni haki ya msingi katika jamii zetu huru. Lakini vipi haki ya kutoa maoni huru inahusiana na kuwatukana waumini wa Kiislamu?”

Na hatimaye tuelekee nchini Ujerumani ambapo waziri wa mazingira Siegmar Gabriel anagonga vichwa vya habari pale anapotaka kusitisha haraka vituo vya kinyuklia vya kutengeza nishati. Kulingana na gazeti la “Volksstimme” la mjini Madgeburg”, waziri huyu ana maslahi mengine:

“Waziri huyu anapigania sana kusitisha matumizi ya nishati ya kinyuklia. Sasa anadai hata vituo saba vifungwe mara moja. Inajulikana kwamba waziri Gabriel anataka kuchukua kiti cha Kansela, lakini anashindwa kufanikiwa katika suala la pili muhimu ambalo ni wadhifa wake, yaani suala la ulinzi wa hali ya hewa. Hapa, Kansela Merkel tayari analishughulikia vizuri. Hata hivyo, kuzima vituo vya kinyuklia vitazidisha tu tatizo la utoaji wa gesi chafu.”