1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Irak miaka mitano baada ya Uvamizi wa Marekani

D.Scheschkewitz/P.Martin20 Machi 2008

Miaka mitano iliyopita,Rais wa Marekani George W.Bush alipoamua kupeleka vikosi vyake nchini Irak,aliungwa mkono na Wamarekani wengi na wakati huo huo alipingwa na takriban ulimwengu mzima.

https://p.dw.com/p/DRgo
President Bush delivers remarks on the "Global War on Terror" Wednesday, March 19, 2008, at the Pentagon. (AP Photo/Gerald Herbert)
Rais George Bush akitoa hotuba yake katika Pentagon kuhusu vita dhidi ya ugaidi.Picha: AP

Wamarekani wakati huo walikuwa katika hali ya bumbuazi kufuatia mashambulizi ya Septemba 2001 na waliweza kusadikishwa na serikali iliyojiamulia kwenda vitani.Miaka hiyo mitano iliyopita,Marekani na washirika wake walipoivamia Irak,ulimwengu kwa haki ulisikitishwa na jinsi wanasiasa wa Marekani kwa msaada wa Idara ya Ujasusi ya Marekani walivyobuni kwamba Irak ilikuwa na silaha za maangamizi na kwa njia hiyo kwenda vitani nchini Irak.Vita hivyo havikusababisha tu vifo vya maelfu ya Wairaki bali Marekani pia ilipoteza uaminifu wake kote duniiani.

Mengi yaliyotabiriwa wakati huo na wapinzani wa vita vya Irak yametokea,lakini utabiri mwingine umekwenda kombo.Kwa mfano waliopanga vita hivyo katika wizara ya ulinzi ya Marekani,-Pentagon na kuamini kuwa nchi kama Irak itaweza kushindwa kwa silaha za kisasa na kudhibitiwa kwa urahisi na wanajeshi wachache tu walikosea.Uvamizi uliofanywa haraka haraka umegeuka kuwa vita vya mpangilio.

Lakini hata wale waliodhani kuwa Irak kamwe haitokuwa na mfumo wa kidemokrasia walikosea.Kwani Wairaki licha ya kukumbana na ugaidi wa mara kwa mara walipiga kura kuchagua rais na bunge lao.Haki hiyo mpya iliyopatikana kwa shida kubwa sasa inatumika nchini humo.Vile vile uchumi wa nchi uliokuwa katika hatari ya kuvurugika miaka michache ya mwanzo,sasa umepata nafuu.Ukuaji halisi wa asilimia 6 si mbaya kwa uchumi wa nchi iliyokumbwa na vita.

Kwa mujibu wa wakuu wa mashirika ya mafuta ya kimataifa, mnamo mwisho wa mwaka uliopita uzalishaji wa mafuta nchini Irak ulifikia kiwango sawa na kile kilichokuwepo kabla ya vita.Sasa umma unanufaika kutokana na utajiri huo baada ya hapo awali kuwepo mizozano ya muda mrefu juu ya njia ya kugawana pato la mafuta,jambo ambalo hatimae litasaidia kuleta hali ya kurdhika nchini.

Vile vile tangu miezi michache iliyopita,hali ya usalama imekuwa bora baada ya Marekani kupeleka vikosi zaidi Irak.Kwa mara ya mwanzo tangu miaka mitano iliyopita,Wairaki wanarejea nyumbani kwa maelfu.Licha ya hali mbaya inayokutikana Irak,maisha chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ni bora kuliko ilivyokuwa wakati wa utawala wa Saddam Hussein.

Nchini Marekani rais mpya atakaechaguliwa mwezi wa Desemba atarithi mzigo wa Bush huko Irak,bila ya kujali ikiwa rais huyo ni kutoka chama cha Republikan au Demokratik.Vile vile hakuna anaetazamiwa kuvirejesha vikosi hivyo nyumbani kwa haraka.Na hilo ni jambo zuri kwani Wairaki wanahitaji msingi wa mpangilio unaoweza kutegemewa na si kuachiwa pengo la usalama.