1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Iran haijali vikwazo"

Maja Dreyer11 Aprili 2007

Maoni ya wahariri leo hasa yanahusu mzozo juu ya mradi wa kinyuklia wa Iran ambao umezuka upya baada ya rais Ahmadinedjad alipoarifu juzi kuwa Iran itaongeza harakati zake za kurutubisha madini ya Uranium. Wahariri wa magazeti ya humu nchini wana wasiwasi juu ya hotuba ya rais Ahmadinedjad.

https://p.dw.com/p/CHTH

Tukianza na mhariri wa “Kölner Stadtanzeiger” ameandika kuwa Ahmadinejad anataka kuwaunganisha Wairan katika hisia za kitaifa. Tunasoma: “Kwa kuonyesha nguvu yake, Iran inataka kuimarisha msimamo wake dhidi ya jumuiya ya kimataifa. Kwa kutangaza mradi wa kinyuklia unafanya kazi, Iran inaweka hali halisi ambayo inazibidi nchi za Magharibi ziikubali – kama ile ya Korea Kaskazini. Wairani wanajua kuwa mzozo unazidi kuwa mkali.”

Lakini mzozo huu utaendelea vipi? Kuna uwezekano wa kuendeshwa vita dhidi ya Iran? Au kwa njia gani mvutano huu utatatuliwa? Ni suala linalozingatiwa na gazeti la Nürnberger Zeitung. Laandika: “Serikali ya siasa kali ya Iran inaonekana inajivunia kwamba imeweza kuzisukuma nchi za Magharibi katika hali isiyo na suluhisho. Ikiwa kweli Iran inapanga kujenga bomu la kinyuklia, basi nchi za Magharibi zina machaguo mawili yote mabaya, yaani kuikubali nchi yenye bomu la kinyuklia au kuanza vita vingine katika eneo la Mashariki ya Kati. Viongozi wa Iran lakini wanajua kuwa Marekani wala Uingereza hazina uwezo wa kuendesha vita vingine kutokana na shughuli zao nchini Iraq na Afghanistan.”

Gazeti la “Rhein-Zeitung” lina matumaini kuwa jibu la jumuiya ya kimataifa linaweza kuwa jibu la pamoja sasa. Mhariri huyu ameandika: “Uchokozi huu mpya wa rais Ahmadinejad ni wa kikaidi mno, kwa hivyo hata China na Urusi zimekubali kuchukua hatua kali zaidi. Huenda vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran vitakuwa vizito zaidi. Vile vikwazo vya aina hii vinaweza kuiathiri nchi, tunaweza kuona nchini Iraq. Mradi wa kinyuklia wa Iran si kitu kisichoweza kuathirika.”

Kinyume na matumaini haya ya “Rhein-Zeitung”, gazeti la “Weser-Kurier” la mjini Bremen linaukosoa msimamo wa jumuiya ya kimataifa katika mzozo huu na Iran. “Inaonekana kama serikali ya Iran haina hofu juu ya vikwazo vilivyokubaliwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, yaani kuzuia biashara ya silaha, safari na fedhi zilizoko katika nchi za nje. Sababu ni kwamba makubaliano haya hayajafuatiwi na hatua za pamoja.”

Licha ya mzozo huu kuwa mkali, gazeti la “Abendzeitung” kutoka Munich linataka mazungumzo ya kidiplomasia yaendelee. Limeandika:
“Lazima makundi yasiyo na msimamo mkali nchini Iran yapewe nguvu na jumuiya ya kimataifa. Hii itawezekana tu kwa kukubali Iran ifanye utafiti wa kinyuklia, jambo ambalo haliwezi kuzuiliwa tena.”

Na hatimaye ni gazeti la Pforzheimer Zeitung ambalo limeandika yafuatayo:
“Mfano huu wa Iran unaonyesha wazi vile Umoja wa Mataifa hauna la kufanya ikiwa nchi inajitenga na mfumo wa kidiplomasia kwa kutojali diplomasia. Sababu nyingine ya mzozo huu na Iran ni kwamba hakuna siasa za kimataifa zinazokosa sheria halali za kutumia nishati ya kinyuklia.”