1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran haiundi bomu la nuklia

4 Desemba 2007

Idara 16 za ujasusi za Marekani zimearifu kitambo kuwa tangu 2003 Iran imeachana na mradi wa silaha za nuklia.

https://p.dw.com/p/CWae
Bush akiwa na makao-rais wa SudanPicha: AP

Ripoti ya Idara ya upelelezi ya Marekani iliotoka jana(International Intelligence Estimate) imefichua kwamba Iran, tangu 2003 imeachana na azma ya kuunda silaha za kinuklia.Taarifa hii inapingana na madai ya serikali ya George Bush ya Marekani kuwa Iran inaunda bomu la kinuklia.

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak,ambae nchi yake ikishirikiana mno na Marekani kuishinikiza Iran kwa vikwazo na vitisho, anakanusha ugunduzi wa ripoti hiyo ya kituo cha upelelezi cha Marekani cha “National Intelligence Estimate (NIE) kwa ufupi.

Hadi sasa serikali ya George Bush ya Marekani ikihanikiza ulimwengu mzima kwamba Mashariki ya kati inahatarishwa na kitisho cha bomu la kinuklia ambalo eti Iran inaunda.Kwa muujibu wa uchunguzi alioufanya mshindi wa zawadi ya uchapishaji habari Seymour Hersh, Bush ameshaandaa mipango ya vita dhidi ya Iran.

Sasa lakini, uongo unajitenga na ukweli unadhihirika ?

Ni miezi 2 hivi nyuma tuhapo oktoba, pale rais George Bush alipouonya ulimwengu kwamba :anaetaka kuepusha vita 3 vya dunia ,aizuwie Iran isiunde bomu la atomiki.

“Ndio, naamini wana nia ya kuunda bomu la kinuklia na ni kwa masilahi ya ulimwengu kuwazuwia wasifanye hivyo.”

Onyo lake hilo halikupita hata wiki 7 tangu alitoe na sasa ukweli unadhihirika kuwa akijua hiyo si kweli.Kwani, tangu 2003 idara za ujasusi za marekani zimearifu kwamba Iran imeachana kabisa na mpango wake wa kuunda bomu la kinuklia.Taarifa hizo zimetolewa na idara zote 16 za ujasusi za Marekani.

Sasa sura ni nyengine kabisa kuliko vile utawala wa Bush ulivyokua ukitoa hadi jana.

Stephen Hadley,mshauri wa usalama wa Taifa wa marekani,anajaribu licha ya ukweli huo kutoa dhana kana kwamba msimamo wa rais Bush na kufichuliwa kwa ripoti hiyo jana kunakwenda sambamba. Hadley adai:

“Kile alichojaribu rais ni kuuzindua ulimwengu kwamba tunapaswa kuongeza shinikizo dhidi ya Iran ili iachane kabisa na mradi wake kwa njia ya kuamirisha madini ya uranium.Hali ni bado iko hivyo.Kwani, mradi huo ni njia ya kwendea shabaha hiyo ya silaha.”

UM kupitia shinikizo la Marekani imeshaiwekea Iran vikwazo mara mbili na unazingatia kifurushi cha tatu cha vikwazo.

Wachunguzi wanauliza iwapo kwa jicho la ripoti ya jana na kwa muujibu wa idara 16 za ujasusi za Marekani,hii inastahiki ?

Israel, imekua mshirika wa chanda na pete wa Marekani katika kueneza hatari inayotoakana na mradi wa kinuklia wa Teheran.Waziri wa ulinzi wa Israel,Ehud Barak amesema leo kuwa Iran pengine imeanzisha upya mradi wake wa silaha ya kinuklia .Ikiwa ni hivyo, waziri wa ulinzi wa Israel,anapinga ripoti za idara 16 za kijasusi za Marekani zinazodai kinyume chake.Iran daima ikidai inatumia ufundi wa kinuklia kwa madhumuni ya amani -ya nishati ya kinuklia.

Katika Mashariki ya kati ni Israel tu inayoaminiwa kumiliki boma la silaha za kinuklia ingawa binafsi haikuwahi kuungama hayo.Utawala wa Bush ulidai Iraq chini ya marehemu Saddam Hussein,ikimiliki silaha za kinuklia. Ilikuja baadae kudhirika si kweli.