1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran inasema haina haja ya kutengeneza silaha za nuklea.

Mohamed Dahman3 Juni 2008

Iran yakanusha vikali madai ya kutengeneza silaha za nuklea wakati shirika la nuklea duniani likitaka nchi hiyo ifichuwe yote kuhusu mpango wake wa nuklea.

https://p.dw.com/p/EC7o
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.Picha: AP

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei leo hii amekataa vikali madai kwamba serikali ya Iran inataka kutengeneza silaha za nuklea huku kukiwa na wasi wasi unaozidi kuongezeka kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya nuklea juu ya harakati za Iran kumiliki silaha hizo za nuklea.

Taifa la Iran halitaki kutengeneza silaha za nuklea hayo ni matamshi ya Khamenei katika hotuba iliotangazwa moja kwa moja leo hii katika runinga ya taifa kwa kumbukumbu ya kifo cha kiongozi wa mapinduzi ya Iran Ayatollah Ruholllah Khomeini mwaka 1989.

Ameongeza kusema kwamba wanachotaka ni kuwa ni nishati ya nuklea kwa ajili ya dhamira za amani kwa matumizi ya kila siku na kwamba wataendelea na mpango huo licha ya wivu wa maadui zao na kwamba kwa uwezo wa mungu watafanikisha lengo hilo.

Khamenei huko nyuma mara kwa mara alikuwa akisema kwamba mpango wa nuklea wa Iran ni kwa ajili ya matumizi ya amani na kwamba silaha za nuklea zinakwenda kinyume na Uislamu.Lakini ukali na ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo katika hotuba yake ya leo ulikuwa sio wa kawaida.

Kauli yake hiyo inakuja baada ya Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Nuklea Mohamed El Baradei kutaka Iran ifichuwe kila kitu juu ya mpango wake wa nuklea kutokana na madai nchi hiyo imeficha habari muhimu juu ya utengenezaji wa silaha katika mpango wake wa nuklea uliozusha utata.

Shirika hilo la IAEA limekuwa likichunguza habari za ujasusi miezi kadhaa iliopita zilizotolewa na mataifa ya magharibi kwamba Iran ilikuwa imejifunza namna ya kutengeneza bomu la nuklea.

IAEA hivi sasa iko katika mkutano wake wa kiangazi wa bodi ya magavana ya wajumbe 35 na mpango wa nukela wa Iran ni suala kuu katika mjadala.

Shirika hilo la nuklea limeelezea wasi wasi mkubwa kwamba Iran ilikuwa ikificha habari juu ya madai ya utafiti wa kutengeneza makombora ya nuklea halikadhalika kukaidi madai ya Umoja wa Mataifa kusitisha urutubishaji wa madini ya uranium.

Lakini Khamenei amesema taifa la Iran kimsingi na kwa sababu za kidini liko dhidi ya silaha za nuklea kutokana na silaha hizo kuwa na gharama kubwa sana na hazina faida kwamba hazileti nguvu kwa taifa.

Khamenei pia ameelezea wasi wasi wake kwamba magaidi kuna siku watatia mkononi mabomu ya nuklea na kusababisha maafa duniani kote.

Marekani na washirika wake wa Ulaya zina hofu kwamba Iran inataka kutumia mchakato nyeti wa kurutubisha uranium kwa ajili ya kutengeneza bomu la nuklea.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeweka aina tatu ya vikwazo dhidi ya Iran kutokana na nchi hiyo kugoma kusitisha urutubishaji wa uranium.

Marekani na mshirika wake wa Mashariki ya Kati Israel hazikufuta uwezekano wa kuchukuwa hatua ya kijeshi dhidi ya Iran kutokana na mpango wake huo wa nuklea.

Al Baradei pia ametangaza kwamba wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wataitembelea Syria kuanzia tarehe 22 hadi 24 mwezi wa Juni kuchunguza madai kwamba serikali ya nchi hiyo ilikuwa ikijenga mtambo wa nuklea ambao haukutangazwa kabla ya kuteketezwa katika shambulio la anga la Israel mwezi wa Septemba mwaka jana.