1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran itaitikia wito wa kuachana na mradi wake wa nyuklia?

Admin.WagnerD16 Julai 2012

Utawala wa Rais Barack Obama umeiwekea Iran na makampuni kadhaa vikwazo vipya vya fedha, hatua iliyochukuliwa hivi karibuni kama sehemu ya kuendelea kuongeza mbinyo kwa taifa hilo la kiislamu.

https://p.dw.com/p/15YE4
Rais Mahmud Ahmadinejag (katikati) akikagua mradi wa kurutubishia madini ya uranium.
Rais Mahmud Ahmadinejag (katikati) akikagua mradi wa kurutubishia madini ya uranium.Picha: AP

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya fedha ya Marekani, makampuni hayo ni yale yanayotuhumiwa kushirikiana na Iran katika kutekeleza mpango wake wa nyuklia na utengenezaji wa makombora ya masafa marefu.

Kitengo hicho kimesema kinayaorodhesha makampuni 11 na watu kadhaa wanaoshirikiana na wizara ya ulinzi ya Iran, shirika la uchukuzi wa meli pamoja na watu kadhaa wenye mafungamano na jeshi la Mapinduzi la Iran.

Miongoni mwa makampuni hayo yaliyoorodheshwa na Marekani yako nchini Uswisi, Malaysia na Hong Kong. Kampuni ya taifa ya magari makubwa ya kubebea mafuta nchini Iran nayo imetajwa katika orodha hiyo ambapo inatuhumiwa kutumiwa na shirika la mafuta la taifa kuepuka vikwazo vilivyowekwa vya kutosafirisha mafuta nje ya Iran.

Vikwazo hivi vitaendelezwa?

Naibu waziri wa fedha David Cohen, amesema kwa sasa Iran inakabiliwa na vikwazo vingi vikali na Marekani itaendelea kuongeza mbinyo madhali taifa hilo linakataa kujibu maswali ya jumuiya ya kimataifa kuhusiana na mpango wake wa nyuklia.

Rais Barack Obama -Taifa lake linafanya kila liwezekanalo kusitisha mradi wa nyuklia wa Iran.
Rais Barack Obama - Taifa lake linafanya kila liwezekanalo kusitisha mradi wa nyuklia wa Iran.Picha: Reuters

Wakati wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani ikiiadhibu Iran kwa jinsi hiyo, wachambuzi wa mambo wanahisi vikwazo hivyo vipya vinaweza kusababisha athari.

Akitoa dukuduku lake, Rais wa Baraza la Taifa la Iran na Marekani NIAC ambaye pia ni mtunzi wa vitabu maarufu juu ya diplomasia ya mataifa hayo mawili, Trita Parsi, amesema swali lililopo kwa sasa ni Je! Ni kwa kiasi gani ongezeko hilo la vikwazo linaweza kuvumiliwa kabla ya mchakato huo wa kidiplomasia haujasambaratika na iwapo itakuwa hivyo...Ni nini kitakachotokea?

Vikwazo hivyo vipya ni muendelezo wa vikwazo vingine vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran mwezi uliopita, baada ya kuidhinishwa na Bunge la Marekani, mwezi Desemba mwaka jana, kuziadhibu taasisi za kifedha za mataifa ya nje ambazo zinafanya biashara na Benki Kuu ya Iran.

Julai mosi mwaka huu marufuku iliyowekwa na Umoja wa Ulaya ya Iran kutopeleka mafuta katika nchi zake wanachama ilianza kutekelezwa.

Kwa upande wake, Iran, wiki iliyopita ilitumia siku tatu kufanya mazoezi ya kijeshi yaliyolenga kuonesha kuwa makombora yake ya masafa marefu yana uwezo, pasi na shaka, wa kuvishambulia vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyopo katika Eneo la Ghuba sawa na maeneo ya Israel.

Kiongozi wa Israel, Benjamin Netanjahu: Iran ishughulikiwe
Kiongozi wa Israel, Benjamin Netanjahu: Iran ishughulikiwePicha: dapd

Vikwazo hivyo vipya na mazungumzo yanayofanywa na Marekani yanashuhudiwa wakati mikutano mikubwa mitatu kati ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiendelea tangu mwezi Machi mwaka huu.

Ni upi msimamo wa Israel?

Kwa kipindi kirefu, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, amekuwa akisisitiza kuwa serikali ya Iran haitakiwi kuruhusiwa kurutubisha madini ya uranium katika eneo hilo.

Wakati rais Obama akionekana kutofika mbali kiasi hicho, kwa sasa anaonekana kuwa na msimamo kama ule wa Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush, ambaye alisisitiza kuwa Iran itapaswa kushinikizwa kusitisha mradi wa kurutubisha madini ya uranium mpaka maswali yaliyoulizwa na Shirika la Kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, kuhusu matumizi ya kijeshi ya mpango huo, yatakapopatiwa majibu.

Vile vile, Marekani inaonekana kuridhia ombi la Israel kutaka kiwanda cha Iran cha urutubishaji wa madini ya uranium cha Fordo kilicho chini ya ardhi, kiharibiwe kabisa kabla ya kuanza kutafakari kuiregezea vikwazo Iran.

Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul/IPS

Mhariri:Josephat Charo