1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: kujenga viwanda kumi vipya vya kurutubisha Uranium

30 Novemba 2009

Ikulu ya Marekani imeonya kwamba muda wa Iran kuyakubali masharti ya jumuiya ya kimataifa unayoyoma, huku Iran ikitangaza itajenga viwanda vingine vikuu vya kurutubisha madini yake ya Uranium.

https://p.dw.com/p/Kki5
Rais Mahmoud Ahmedinejad asema hakuna atakayezuia haki ya Iran ya kuwa na mradi wa nuklia.Picha: AP

Na si Marekani tu, Ufaransa na Ujerumani pia zimeelezea wasiwasi wao, kufuatia tangazo la Iran, huku Ujerumani ikisema Iran haina budi kuyakubali masharti ya jumuiya ya kimataifa kuhusiana na mpango wake wa nuklia na pia kushirikiana kikamilifu na shirika la kudhibiti silaha za atomiki, IAEA. Munira Muhammad ana taarifa kamili.

Hata kabla ya tangazo la ujenzi wa viwanda vipya, tayari hali ya kutoaminiana kati ya Tehran na nchi za Magharibi ilikuwa imejitokeza. Jumuiya ya kimataifa ilikuwa imekasirishwa na uamuzi wa Iran kulikatalia mbali lile pendekezo la kusafirisha madini yake ya Uranium ili yarutubishwe nje ya nchi hiyo.

Iran - Atomkraftwerk Buschehr
Iran kujenga viwanda kumi vya kurutubisha madini ya Uranium.Picha: ISNA

Na jana, unga ukazidi maji. Baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na Rais Mahmoud Ahmedinejad, hili ndilo lilikuwa tangazo- Iran kujenga viwanda kumi vipya kuanza shughuli ya kurutubisha madini yake ya Uranium.

Agizo hilo la baraza la mawaziri, likaweka ratiba ya kuanza ujenzi wa vinnu vyake vitano katika miezi miwili ijaayo, huku wakisaka maeneo mengine muafaka ya kujenga viwanda vitano vilivyosalia. Spika wa bunge Ali Larijani katika mkutano na waandishi wa habari alisema uamuzi wa Iran uliafikiwa kutokana na vitisho walivyopata, hapa akiitaja Israel.

'' Tulipokuwa tunaendelea kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhdibiti silaha za nuklia IAEA, kuhusiana na upatanishi wa mradi wetu wa nuklia, Israel ilikuwa inatutolea vitisho, ni vitisho hivyo ndivyo vimesababisha sisi kutafuta suluhisho jingine ili kuilinda haki yatu ya kuwa kuwa na mradi wa nuklia." Alisema Larijani.

Jumuiya ya kimataifa nayo haikusubiri kutoa majibu yake. Ikulu ya Marekani ilionya muda unayoyoma kwa Iran kurejesha imani yake kwa jumuiya ya kimataifa. Msemaji wa Ikulu hiyo Robert Gubbs alisena nikimnukuu,

Amerika Barack Obama Solar Energie Zentrum
Rais Barack amekuwa akiinyoshea Iran mkono.Picha: picture-alliance/ dpa

'' Kama taarifa hizi ni za kweli, hii itakua hatua nyingine ya Iran kukiuka jukumu lake chini ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa, na ni mfano mwingine Iran imechagua kuendelea kujitenga.'' Mwisho wa kumnukuu.

Ujerumani ilielezea wasiwasi wake ikisema Iran inawajibika kuridhia masharti ya jumuiya ya kimataifa na kushirikiana kikamilifu na shirika la kudhibiti silaha za atomiki, IAEA.

Tangazo la jana kutoka Iran, linakuja siku mbili tu baada ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kudhibiti silaha za nuklia IAEA, kupitisha kwa pamoja azimio la kuilaani Iran kwa kubana taarifa za kuwepo kwa kiwanda chake cha kurutubisha madini cha Fordo karibu na mjii mkuu, Tehran.

Akijibu azimio hilo, Rais Ahmedinejad akwa mara nyingine tena alisema Iran haitoruhusu yeyote kuinyima haki yake ya kuwa na mradi wa nuklia.

Na si hayo Iran iimetishia huenda ikaacha kushirimki katika mazungumzo kuhusu mradi wake wa nuklia yanayoongozwa na shirika hilo la kudhibiti silaha za atomiki.

'' Iwapo hamtositisha sera za kunyoosha mkono na vitisho vile vile, Iran haitakuwa na budi ila itaamua kuwa na sera mpya ya kupunguza ushirikiano wake katika mazungumzo yake na shirika la kudhibiti silaha za atomiki , IAEA, alisema spika wa bunge Ali Larijani.

Mwandishi: Munira Muhammad/ DPAE

Mhariri: Abubakary Liongo.