1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Kuna nini kipya?

11 Aprili 2007

Tangu rais Ahmadinejad wa Iran alipotangaza kuwa nchi yake sasa inaweza kurutubisha madini ya Uranium katika viwanda vyake, majibu ya jumuiya ya kimataifa yalikuwa tofauti. Si dhidi ya sheria inyoipa haki Iran iwe na nishati ya nyuklia, lakini nchi nyingi haziamini kuwa Iran itatumia nishati hiyo kwa ajili ya kutengeneza umeme tu, bali zinaamini Iran inapanga kutengeneza mabomu ya kinyuklia. Mwandishi wetu na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, Peter Philipp, ameandika uchambuzi juu ya mzozo huu.

https://p.dw.com/p/CHGT

Je, kuna nini kipya? Hivyo tungeweza kuuliza pale rais Mahmud Ahmadinejad wa Iran alipoarifu kuwa nchi yake inaweza kurutubisha Uranium kwa kiwango cha kiviwanda na hivyo nchi hiyo kuwa ni moja kati ya mataifa yanayotumia nishati ya kinyuklia. Lakini swali hili halikusikika. Badala yake, watu wengi waliuona huo ni uchokozi mpya dhidi ya nchi za Magharibi na waliwaza lini Iran itaweza kutengeneza bomu lake la kwanza la kinyuklia. Wengine waliidhihaki Iran na kusema Iran bado haiko tayari kwa hatua hiyo na kwamba rais Ahmadinejad alisema uwongo, kama mchezaji mzuri wa tamthilia.

Hata ikiwa majibu haya ni tofauti kabisa, yanaonyesha tu kuwa dunia haijui la kufanya kuhusiana na Iran. Wataalamu pia wanatoa maoni ya juu juu tu, wakizungumzia Iran na hawana habari zaidi Iran imefika wapi katika mradi wake wa kinyuklia.

Katika hali hii inapaswa kuwa na utulivu na unyamafu zaidi. Bomu la kinyuklia la Iran liko tu katika vichwa vya wale watu ambao wana wasiwasi juu ya serikali ya Iran na namna serikali hiyo inavyounganisha siasa na dini ya Uislamu. Au kwa nini Iran inafikiriwa kuwa na lengo la kutengeza bomu la kinyuklia licha ya kuwa imehakikisha mara nyingi inataka kutumia tu umeme kutoka vituo vya kinykulia na pia Iran kutia saini mkataba dhidi ya silaha za kinyuklia? Na kwa nini hakujafanywa juhudi zozote kuzishawishi nchi nyingine za Mashariki ya Kati ambazo hazijatia saini mkataka huo zikubali kutotumia silaha za nyuklia?

Matatizo ya sera na jumuiya ya kimataifa yanaonekana pia tukikumbuka kuwa nchi nyingine haziilaumu Iran kwa kurutubisha Uranium – kitu ambacho kisheria Iran inaruhusiwa kufanya. Lakini zinailaumu Iran kwa kutotimiza masharti ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lakini lina dai ambalo si sawa, yaani kuachana na mradi wa kurutubisha Uranium.

Lile ambalo ni zuri sasa hivi ni kwamba bado kuna watu wanaodai mazungumzo na Iran yaanzishwe. Lakini bila ya kuwa na kitu cha kuipa Iran mazungumzo hayo hayawezekani, wala kwamba nchi ambazo zinataka vikwazo dhidi ya Iran viongezwe zinazungumza na Iran. Inabidi nchi za Magharibi bila ya fikra kuwa na mbaya, ziseme ukweli na zisiweke masharti yasiyo halali – pale tu inapokuweko fursa kwamba hali inaweza kutulia.

Hakuna uhakika kuwa Iran haitatengeneza bomu la kinyuklia. Lakini hali ya kuaminiana itachangia vikubwa kuleta suluhisho.