1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na madini ya Uranium.

Halima Nyanza24 Mei 2010

Iran leo imekabidhi barua kwa waangalizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki makubaliano ya kusalimisha madini yake ya Uranium yaliyorutubishwa.

https://p.dw.com/p/NVqS
Mkuu wa programu ya nyuklia ya Iran, Ali Akbar Salehi.Picha: ISNA
Barua iliyosainiwa na Mkuu wa programu ya nyuklia ya Iran, Ali Akbar Salehi, imekabidhiwa kwa Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic -IAEA- Yukiya Amano katika mkutano uliodumu takriban dakika 45 mjini Vienna, Austria. Televisheni ya Taifa ya Iran imenukuu barua hiyo kwa kusema kuwa makubaliano hayo ni hatua kubwa kuweza kumaliza hofu juu ya mpango huo. Vyombo vya habari nchini Iran vimesema pia barua hiyo itakuwa mwanzo wa majadiliano zaidi juu ya kubadilishw mafuta kupitia kusainiwa kwa makubaliano. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo la  Atomiki, Mkurugenzi mkuu ataipeleka barua hiyo Marekani, Ufaransa na Urusi ili nchi hizo ziweze kuizingatia. Nchi hizo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa awali chini ya mkuu wa zamani wa shirika hilo la Atomiki, Mohamed ElBaradei, yaliyofikiwa Oktoba mwaka jana, lakini hayakufanikiwa kufuatia matakwa ya Iran kufanyike marekebisho. Pendekezo hilo juu ya kubadilisha madini ya uranium yaliyorutubishwa kwa kiwango cha chini -LEU- kwa mafuta kwa ajili ya kuweza kuendesha maabara ya Iran ya utafiti wa matibabu, ambalo linalenga kuondoa hofu kwamba Iran inataka kujipatia madini hayo kwa ajili ya silaha za nyuklia, lilifikiwa wiki iliyopita na nchi hiyo pamoja na Uturuki na Brazil. Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Uturuki na Brazil walitia saini makubaliano yanayojumuisha Iran kutuma kiasi cha kilo 1,200 ya madini yake ya Uranium kurutubishwa nchini Uturuki na baadaye yarejeshwe nchini Iran kutumiwa katika matumizi ya nishati. Akizungumza awali kuhusiana na nchi yake ilivyotayari kutoa ushirikiano na jumuia ya kimataifa, Mkuu wa programu ya nyuklia ya Iran, Ali Akbar Salehi. alisema katika nia yao njema na kuonesha utayari wao wa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu za Atomiki, wamekubali kufanya mabadilishano kufuatana na utaratibu ambao ulishikiliwa na nchi za magharibi, nao ni kukubali kukabidhi madini ya nchi hiyo yasiyosafishwa kwa nchi ya tatu. Hata hivyo, mataifa ya magharibi yanaona makubaliano hayo yanalingana na yale ambayo Iran ilijitoa miezi sita iliyopita. Iran ilitishia kuacha kutekeleza mpango huo iwapo itakumbwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyozingatiwa kuchukuliwa mwezi ujao. Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters) Mhariri: Miraji Othman