1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na nchi zenye nguvu hazijakubaliana

19 Machi 2015

Maafisa walioko kwenye mazungumzo ya Lausanne nchini Switzerland ya mpango wa Nyuklia wa Iran wanasema rasimu ya makubaliano inayojadiliwa itailazimu Iran kupunguza kwa kiasi kikubwa urutubishaji wa madini ya Urani

https://p.dw.com/p/1Eu3q
Wajumbe wanaojadiliana Lausanne Switzerland
Wajumbe wanaojadiliana Lausanne SwitzerlandPicha: Isna

Leo 19.03.2015 ni siku ya nne ya mashauriano ya kina juu ya mpango wa Nyuklia wa Iran na kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif hatua zimepigwa lakini yapo mengi pia ya kuangaliwa,tathmini ambayo pia imeungwa mkono na mwenzake wa Marekani John Kerry.

Kerry amesema mashauriano hayo yanakabiliwa na masuala mazito ingawa pia kuna hatua zilizopigwa kuelekea tarehe ya mwisho iliyowekwa ya kupatikana makubaliano kamili tarehe 31 mwezi huu wa Marchi.Maafisa wanasema rasimu ya makubaliano inayojadiliwa itaizuia Iran kurutubisha madini ya Urani kwa kiwango alau cha 40 asilimia kwa muda wa muongo moja au zaidi.

Lakini kwa upande mwingine maafisa wanasema rasimu hiyo itaipa pia nafasi Iran ya kuondolewa vikwazo ambavyo vimeudhoofisha uchumi wake.Hata hivyo mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya anayehusika kwenye mashauriano hayo amesema kwamba Iran na nchi sita zenye nguvu ambazo ni Marekani,China,Urusi,Uingereza,Ufaransa na Ujerumani bado zipo mbali kufikia maridhiano kwasababu Iran inaoekana kurudi nyuma na kwenda mbele katika mazungumzo hayo,kwa ufupi inabadili msimamo kila wakati.

Marekani huenda ikatangaza vikwazo vipya,mazungumzo yakishindwa
Marekani huenda ikatangaza vikwazo vipya,mazungumzo yakishindwaPicha: Isna

Aidha mjumbe huyo amesema hatarajii kwamba kufikia kesho makubaliano yatafikiwa,muda ambao ulipangwa wa mazungumzo ya wiki hii kumaliziza na kwahivyo basi kuna uwezekano mkubwa wa wajumbe hao kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo wiki ijayo.Marekani lakini imeshatoa ishara kwamba haiwezi kuvumilia muda wa mazungumzo kuongozwa kila wakati ambapo Afisa mmoja mwandamizi katika wizara ya fedha ametoa kauli leo kwamba serikali ya Obama itashirikiana na bunge kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran ikiwa makubaliano hayatofikiwa.Tokea hapo wapinzani wa Obama wa chama cha Republican wanazungumzia juu ya bunge kuweka vikwazo vipya ambavyo vinaweza kuyavunja kabisa mazungumzo hayo.

Chama cha Republican na waziri mkuu aaliyechaguliwa tena madarakani nchini Israel Benjamin Netanyahu ambaye nchi yake kwa kiasi kikubwa inafikiriwa kuwa na silaha za Nyuklia wanakhofia makubaliano kati ya Iran na nchi zenye nguvu hayatoizuia Iran kutengeneza bomu. Rasimu ya makubaliano inayojadiliwa na ambayo inategemewa kukamilishwa kufikia Julai inanuiwa kuushawishi ulimwengu baada ya kuwepo mvutano huu wa Nyuklia kwa miaka 13 sasa na khofu kwamba Iran itatengeneza sialaha za maangamizi makubwa kwa kisingizio cha mpango wake wa Nyuklia wa matumizi ya kawaida.Mpaka sasa wajumbe wanaoshiriki mazungumzo hayo wameshindwa mara mbili mwezi Julai na Novemba kufikia makubaliano hadi muda wa mwisho uliowekwa licha ya kufanyika duru kadhaa za mazungumzo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/afpe/APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman