1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran sasa ina uwezo wa kurutubisha madini ya uranium kwa kiwango kikubwa

10 Aprili 2007

Rais Ahmadinejad wa Iran ametangaza kwamba nchi yake sasa ina uwezo wa kurutubisha madini ya uranium kwa kiwango kikubwa. Hatua hiyo imesababisha wasi wasi juu ya Iran kuwamo katika njia ya kuunda silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/CB4o
Rais Ahmadinejad wa Iran
Rais Ahmadinejad wa IranPicha: AP

Akizungumza katika maadhimisho ya mwaka mmoja tokea nchi yake ianze kurutubisha madini hayo kwa mafanikio, rais Ahmadinejad aliimbia dunia kwamba nchi yake sasa ina uwezo wa kuyachuja madini ya uranium kwa kiwango kikubwa. Bwana Ahmadinejad pia ametetea haki ya nchi yake katika kuendeleza tekinojia ya kinyuklia kwa madhumuni ya amani.

Iran imeingia katika hatua hiyo wakati ambapo kiasi cha wiki mbili tu zilizopita, baraza la usalama lilipitisha azimio, kuitishia Iran na vikwazo vikali endapo haitaacha shughuli za kurutubisha madini ya uranium mnamo muda wa siku 60.

Hatua hiyo ya Iran ya kuweza kuzalisha kurutubisha madini ya uranium kwa kiwango kikubwa imesababisha wasi wasi duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Ban Ki- moon amesema anatumai kuwa nchi hiyo itakuwa tayari kufanya mazungumzo.

Bwana Ban Ki.moon ameeleza kuwa hata sasa, wakati ambapo Iran inakabiliwa na vikwazo ingelifaa kwa serikali ya nchi hiyo kufanya mazungumzo. Na ametoa mwito kwa serikali ya Iran juu ya kuheshimu maazimio yote ya Umoja wa Mataifa.

Na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Sean McCormack ameeleza kuwa hatua ya Iran kuanza kuzalisha madini ya Uranium kwa kiwango kikubwa inaenda kinyume na kanuni za jumuiya ya kimataifaBwana McCormack amesema kuwa Iran imepoteza nafasi nyingine.

Hii ni fursa nyingine iliyopotea. Katika miezi iliyopita Iran ilipewa fursa kem kem za kufanya mazungumzo juu ya uwezekano wa kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani.

Na msemaji wa Umoja wa Ulaya ametoa miito mingine kwa Iran juu ya nchi hiyo kuacha kurutubisha madini ya Uranium.

Lakini mjumbe wa kimataifa wa Iran bwana Ali Larijani amejibu lawama hizo kwa kuonya kuwa huenda Iran ikaangalia upya msimamo wake juu ya mkataba wa kuzuia uenezaji wa nishati tekinolijia nyuklia duniani.

Na ABDU MTULLYA