1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaashiria haina mpango wa kujibu shambulizi la Israel

Daniel Gakuba
20 Aprili 2024

Afisa wa ngazi ya juu wa Iran amesema kuwa nchi hiyo haina mpango wa kulipiza kisasi kwa kile kinachoelezwa na vyanzo vya habari kuwa shambulizi la Israel katika mji wa Isfahan usiku wa kuamkia Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4f00b
Iran, Teheran | Graride la zana za kivita
Gwaride la zana za kivita mjini Tehran nchini IranPicha: Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Afisa huyo ambaye jina lake halikutajwa, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kilichotekea ni hujuma za kujipenyeza kuliko kuwa mashambulizi yanayoripotiwa na vyanzo vya kigeni. 

Hata waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amirabdollahian, akizungumza na wajumbe wa mataifa ya Kiislamu mjini New York, amesema mashambulizi yalifanywa na dronindogo na hayakusababisha uharibifu wowote. 

Israel haijatoa taarifa yoyote juu ya mashambulizi hayo inayoripotiwa kuyafanya, na mshirika wake mkuu, Marekani imekataa kujihusisha. 

Soma pia:Iran na Israel zatolewa miito ya kutotanua mzozo wa katika eneo la Mashariki ya Kati

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amefanya mazunguzo na mwenzake wa Israel, lakini taarifa kutoka mazungumzo yao imesema kuwa wamejadili masuala ya kupunguza mivutano, bila kuitaja Iran.

Israel yasema imeruhusu msaada zaidi kuingia Gaza

Israel imearifu jana Ijumaa kuwa imeongeza juhudi za kuingiza misaada ya kiutu kwa wakaazi wa Gaza. Malori 276 yaliyobeba chakula na dawa yaliingia katika Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi, ikiwa ni kwa mujibu wa mamlaka inayohusika na mawasiliano na Wapalestina, COGAT. 

Mzozo | Ukanda wa Gaza | Israel | Malori yaliobeba misaada ya kiutu
Picha hii iliyotolewa na jeshi la Israel tarehe 12 Aprili 2024 inaonyesha malori yaliyobeba misaada ya kibinadamu yakijiandaa kuingia Ukanda wa Gaza.Picha: Israeli Army via AFP

Aidha, paleti 144 za chakula zilidondoshwa kutokea angani, na malori mengine 700 yanasubiri nyuma ya kituo cha ukaguzi cha Kerem Shalom, tayari kuchukuliwa na mashirika ya msaada ya Umoja wa Mataifa ya kusambaza chakula. 

Kutokana na janga la kibinadamu linalowatishia watu wa Gaza, Israel imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka washirika wake wa magharibi na Umoja wa Mataifa, kuitaka iruhusu haraka kuingizwa kwa shehena zaidi za msaada. 

Soma pia:Israel yaendeleza mashambulizi katika ukanda wa Gaza

Ingawa mashirika ya wahisani yametambua ongezeko la msaada unaoingia Gaza, yanasisitiza kuwa bado malori yanayoruhusiwa kuingia hayatoshi, na kulalamika kuwa mapigano yanayoendelea yanakwamisha usambazaji wa msaada unaowasilishwa.