1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakabiliwa na shinikizo za kimataifa kufuatia ghasia za kupinga matokeo ya uchaguzi wa tarehe kumi na mbili mwezi huu.

24 Juni 2009

Watu kumi na saba wanaripotiwa kuuwawa kwenye ghasia hizo na wengine wengi kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/IY9T
Rais wa Marekani Barack Obama.Picha: AP

Iran inaendelea kukabaliwa na shinikizo zaidi za kimataifa baada ya rais wa Marekani Barack Obama kuhoji jinsi serikali ya Iran inavyokabiliana na na ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini humo, kufuatia uchaguzi wa urais uliomrejesha madarakani rais Mahmoud Ahmadinejad.Obama alizungumzia hali ya Iran katika mkutano wake na waandishi habari jana mjini washington.

Iran imekataa kuyatupilia mbali matokeo ya uchaguzi yaliyomrejesha madarakani rais Mahamoud Ahmadinejad lakini hata hivyo kiongozi wa Iran Ayotollah Ali Khamenei ameongeza siku tano zaidi ili kutoa muda wa kusikilizwa kwa malalamiko yanayohusiana na matokeo hayo.

Wakati huo huo mgombea mmoja aliyeshindwa Mohsen Rezai ameondoa malalamiko yake kuhusu matokeo hayo, hatua ambayo inaonekana kama pigo kwa upinzani ambao umefanya maandamano tangu uchaguzi huo kumalizika tarehe 12 mwezi huu.

Hali ya usalama pamoja na ya kisiasa nchini Iran imefikia kiwango cha kuchukua uamuzi, alisema Rezai kwenye barua aliyoliandilia baraza linalosimamaia uchaguzi nchini Iran.

Jana Jumame rais wa Marekani Barack Obama alitoa matamshi makali kuhusiana na uwajibikaji wa uchaguzi wa Iran na kusema kuwa Marekani pamoja na jamiii ya kimataifa wamekasirishwa na kile alichokitaja kuwa vitisho , kupigwa na kufungwa kwa waandamanaji siku chache zilizopita.

Obama alikitaja kuwa kitendo cha kuhuzunisha baada ya dada mmoja kwa jina Neda aliyeuawa kwa kupigwa riasi mjini Tehran na ambaye picha zake zimesambazwa kupitia mtandao kote duniani.

Hata hivyo Iran imeyashutumu mataifa ya kigeni zikiwemo nchi za magharibi kama Marekani na Uingereza kwa kuingilia maswala yake ya ndani.

Uingereza ilisema kuwa ilikuwa inawafukuza waakilishi wa kibalozi wawili wa Iran baada ya Iran kuchukua hatua kama hizo za kuwatimua waakilishi wawili wa uingereza.

Uingereza ambayo pia ilitajwa na kiongozi wa Iran Ayatollah Khamenei kuwa adui mkubwa wa Iran pia inaziondoa familia za wafanyazi wa ubalozi wa uingereta nchini Iran huku nchi zingine za ulaya zikiwaonya raia dhidi ya kusafiri kwenda Iran.

Vyombo vya habari vya kitaifa nchini Iran vinasema kuwa watu 17 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa kwenye ghasia ambazo zimeshihudiwa nchini Iran tangu kumalizika kwa uchaguzi.

Ghasia hizo zinatajwa kuwa mbaya zaidi tangu mapinduzi yaliyofanyika mika 30 iliyopita na kuutikiza utawala wa vingozi wa kidini. Baraza linalohusika na usimamizi wa uchaguzi lenye wanachama 12 linashikilia msimamo kuwa matokeo ya uchaguzi huo yatabakia vile yalivyo.

Baraza hilo hata hivyo lilikiri kuwa kulihesabiwa kura zaidi ya idadi ya wapiga kura waliosajiliwa katika maeneo bunge 50 kati ya maeneo bunge 366 lakini likakataa kuwepo kwa udanyanyifu mkubwa.

Hata hivyo mshindani mkubwa wa rais Ahmadinejad Hossein Mousavi alitoa ripoti iliyoelezea udanganjifu kwenye uchaguzi huo uliompa asilimia 34 dhidhi ya asilimia 63 ya rais Ahmadinejad.

Katika ripoti hiyo Mousavi alitaka kuwepo kwa tume yahaki isisyoegemea upande wowote kuchunguza zoezi lote la uchaguzi huo. Hata hivyo mapema hii leo kulishuhudiwa utulivu katika mitaa ya Iran siku mbili baada ya mandamano kuvunjwa na polisi wa kupambana na ghasia siku ya Jumatatu.

Mwandishi :Jason Nyakundi/AFP

Mhariri : M.AbdulRahman