1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yataka kumaliza mgogoro wa nyuklia

25 Septemba 2013

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema katika baraza kuu la umoja wa Mataifa kwamba yuko tayari kushiriki katika mazungumzo kuhusu mpango wa nchi yake wa kinyuklia na kuwa mpango huo sio tisho kwa jumuiya ya kimataifa

https://p.dw.com/p/19oAg
Picha: Reuters

Katika hotuba kwenye baraza kuu la umoja wa Mataifa,Obama amesema angependa kumuona mwenzake wa Iran akichukua hatua madhubuti kuhusu kuutatua mzozo wa muda mrefu unaohusu mpango wa kinyuklia wa nchi yake ambao umezua utata kati ya Iran na nchi za magharibi.

Saa chache baadaye Rouhani alitumia hotuba yake ya kwanza kama kiongozi wa nchi katika baraza hilo la umoja wa Mataifa kuahidi kuwa Iran ina nia ya kushiriki mara moja katika mazungumzo kuhusu mpango huo wa kinyuklia.

Rouhani amerudia malalamiko mengi ambayo Iran inayo dhidi ya Marekani na mshrika wake mkubwa katika kanda ya mashariki ya kati Israel na kushutumu kuwekwa kwa vikwazo chungu nzima dhidi ya nchi yake na mataifa ya magahribi.

Rais huyo wa Iran na Obama walitarajiwa kukutana ana kwa ana pembezoni mwa mkutano huo wa viongozi wa dunia mjini New York lakini hilo halikuwezakana.Rouhani amesema hakukutana na mwenzake wa Marekani kwa sababu hapakuwepo muda wa kutosha kuandaa mkutano wa aina hiyo.

Rais Barrack Obama akilihutubia baraza kuu la umoja wa Mataifa
Rais Barrack Obama akilihutubia baraza kuu la umoja wa MataifaPicha: Reuters

Rouhani amesema mazingira yanabadilika kwani wa-iran wanataka enzi mpya ya mahusiano na watu kutoka sehemu nyingine za dunia.Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani amesema kushindwa kwa viongozi hao wawili kukutana kulitokana na vipingamizi kutoka upande wa Iran.

Bado kuna mashaka kati ya Iran na Marekani

Kukosekana kwa fursa ya viongozi hao hata kusalimiana kwa mikono inaonyesha ishara kuwa bado ni vigumu kwa nchi hizo mbili ambazo zimekuwa hasimu kwa muda mrefu kufungua ukurasa mpya wa mahusiano.

Mkutano kati yao japo mfupi ungekuwa muhimu kihistoria ikizingatiwa kuwa ungekuwa wa kwanza kwa marais wa nchi hizo mbili kuonana ana kwa ana tangu mapinduzi ya kiislamu yaliyomg'oa madarakani mfalme Shah mwaka 1979 ambaye alikuwa akiungwa mkono na Marekani.

Israel yaibeza hotuba ya Rouhani

Na huku rais Obama akiukaribisha msimamo wa wastani wa Rouhani,waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ulimwengu usidanganywe na maneno matamu ya Rouhani.Kiongozi huyo wa Israel amesema Iran inajaribu kufunika njama yake ya kutengeneza bomu la kinyuklia madai ambayo Iran imeyakanusha:

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle alikutana na Rais huyo wa Iran jana na kukaribisha msimamo mpya wa Iran lakini akasisitiza hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kuhusu mpango huo wa kinyukilia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: MACDOUGALL/AFP/Getty Images

Westerwelle aliisifu hotuba ya Rouhani na kusema ni siku nzuri kwa wanaotafuta suluhisho la kisiasa na kidiplomsia kuhusu Iran.

Wanadiplomsia wamesema mkutano kati ya Westerwelle na Rouhani uliangazia mpango huo wa kinyuklia na vita vya Syria.

Westerwelle atashirki katika mazungumzo ya ngazi ya juu hapo kesho na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka Marekani, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Iran kuhusu mpango huo wa kinyuklia wa Iran.

Waziri huyo wa Ujerumani anatarajiwa kulihutubia baraza la umoja wa Mataifa Jumamosi hii katika kile kinachoonekana kuwa hotuba yake ya mwisho kama waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani kwani anatarajiwa kujiuzulu baada ya chama chake kushindwa katika uchaguzi mkuu

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba