1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yataka mazungumzo na Marekani bila masharti

20 Januari 2012

Umoja wa Falme za Kiarabu umetahadharisha dhidi ya kutokea machafuko zaidi juu ya mgogoro uliopo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, huku Iran ikitaka majirani zake wa Kiarabu kujitenga na Marekani.

https://p.dw.com/p/13nA5
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi.Picha: dapd

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Ali Akbar Salehi, amesema amani na uthabiti wa eneo hilo ndio nia ya nchi hiyo lakini akaonya mataifa jirani kutojiweka katika hali ya hatari kwa kujiweka karibu sana na Marekani. Majirani wa nchi za Kiarabu wa Iran ni washirika wakuu wa Marekani wanaosema kwamba hawatakubali hatua yoyote ya kufunga mlango wa bahari ya Hormuz.

Ali Akbar amesema Marekani inapaswa kujitokeza wazi wazi na kusema iwapo ina nia ya kufanya mazungumzo na Tehran, na inapaswa kufanya hivyo bila ya kuwawekea vikwazo vyovyote. Waziri huyo aliyasema haya baada ya kupokea barua kutoka kwa Rais Barack Obama wa Marekani juu ya kufungwa kwa mlango wa hormuz. habari zaidi juu ya barua hiyo bado haijatolewa. Ikulu ya Marekani imekataa pia kutoa maoni juu ya barua hiyo.

Kwa sasa kuna hali ya wasiwasi kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wake wa nuklia, ambapo Marekani na mataifa mengine yenye nguvu duniani wanasema Iran ina nia ya kutengeneza silaha hizo za atomiki jambo ambalo Iran inakanusha Vikali.

Iran imetishia kufunga mlango wa bahari ya Hormuz ambayo hutumika sana katika kusafirisha mafuta, iwapo mataifa ya Ulaya yatasisitiza nchi hiyo kuwekewa vikwazo katika biashara zake na pia kuzuiliwa kwa mali zake katika benki kuu nchini humo. Iwapo Iran itatekeleza onyo hilo la kuufunga mlango wa bahari ya Hormuz basi kunaweza kutokea mgogoro mkubwa katika jamii ya Mashariki ya Kati.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Hata hiyo, mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana siku ya Jumatatu kukubaliana juu ya ya vikwazo dhidi ya Tehran. Iwapo vikwazo vipya vya Marekani vilivyowekwa saini na rais wa nchi hiyo Barrack Obama siku ya mkesha wa mwaka mpya vitapitishwa, haitaruhusu mataifa mengine kulipia mafuta ya Iran.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nguvu za Atomiki amesema ni jukumu lake kueleza dunia kuhusu uwezekano wa hatua za kijeshi juu ya mpango wa nuklia wa Iran akiweka msisimko mkubwa kabla ya mkutano wa wanachama wa shirika hilo utakaofanyika Januari 29 hadi 31. Nalo shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kitu wanachokijua kwa sasa ni kuwepo kwa harakati za kutengeneza silaha za nyuklia na kwa sasa wanataka kufanya kila juhudi kujua undani wa habari hiyo.

Mwandishi: Amina Abubakar
Mhariri: Yusuf Saumu