1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatangaza ushindi dhidi ya Marekani

Josephat Charo5 Desemba 2007

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ametangaza ushindi baada ya ripoti ya ujasusi kuhusu mpango wake wa nyuklia kutolewa na Marekani. Urusi yasema haja ya kuiwekea vikwazo vipya Iran yapungua.

https://p.dw.com/p/CXYr
Rais wa Iran Mahmoud AhmadinejadPicha: AP

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad ametangaza ushindi mkubwa dhidi ya Marekani hii leo kufuatia kutolewa kwa ripoti ya ujasusi inayosema Iran iliachana na mpango wa kutengeneza bomu la nyuklia tangu mwaka wa 2003.

Ripoti hiyo iliyotolea na jopo la ujasusi la kitaifa, NIE, inaenda kinyume na madai ya serikali ya rais George W Bush kwamba Iran inafanya juhudi za makusudi kutengeneza bomu la nyuklia.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika mkoa wa Ilam nchini Iran, rais Ahmadinejad amesema ripoti hiyo inajaribu kuitoa Marekani kutoka kwa matatizo yanayoikabili lakini wakati huo huo ni tangazo la ushindi wa umma wa Iran dhidi ya nchi zenye uwezo mkubwa duniani.

Aidha kiongozi huyo ameongeza kusema na hapa namnukulu, ´Kupitia msaada wa mwenyezi Mungu, watu wetu wamepinga, wanapinga na wataendelea kupinga hadi mwisho. Nyinyi ni washindi katika nyanja mbalimbali hususan katika swala la nyuklia, ´ amesema rais Ahmadinejad wakati wa hotuba yake iliyoonyeshwa moja kwa moja katika televisheni ya kitaifa.

Akiileza ripoti hiyo kuwa pigo kubwa la mwisho kwa matumaini ya nchi za magharibi, rais Ahmadinejad amewashutumu maadui wa Iran kwa kutaka kuinyima haki ya kumiliki nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia wakati nishati asili itakapomalizika katika kipindi cha miaka 50 ijayo. Lakini rais Bush bado anasema Iran ni hatari.

´Bado ninahisi Iran ni tishio. Hakuna kilichobadilika katika ripoti ya NIE. Wanasema tuache kuwa na wasiwasi juu ya Iran lakini kinyume cha hayo nadhani NIE inaweka wazi kuwa kuna haja ya kuiangalia kwa makini Iran kama kitisho kikubwa kwa amani.´

Rais pia amesisitiza kw akusema, ´Niliamini kabla ya ripoti ya NIE kwamba iran ilikuwa hatari na naamini hata baada ya kutolewa ripoti hiyo kwamba Iran bado ni hatari.´

Jopo la ujasusi la Marekani, NIE, katika ripoti yake lilisema Iran inajaribu kutengeneza nyenzo zinazoweza kutumiwa kutengezea silaha za nyuklia. Ndio maana rais Bush akasema ripoti hiyo ni onyo.

´Naiangalia ripoti hii kama onyo. Wairan wamekuwa na mpango wa kutengeneza bomu la nyuklia lakini wakausimamisha. Sababu kwa nini nasema ripoti hii ni onyo ni kwamba mpangomhuo wanaweza wakauanzisha tena.´

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, akiwa ziarani mjini Addis Ababa, Ethiopia, ameilaumu Iran kwa kuikandamiza demokrasia baada ya kutangaza ushindi dhidi ya Marekani kuhusiana na ripoti juu ya mpango wa nyuklia. Amesema kutolewa kwa ripoti ya jopo la NIE kunaonyesha maana ya kuishi katika demokrasia na kuongeza kusema ana matumaini siku moja Wairan wataishi katika demokrasia.

Hii leo Urusi imejiunga na China kusema ripoti ya jopo la NIE inapunguza haja ya kuiongezea vikwazo Iran. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema mjini Moscow hii leo kwamba Urusi inajaribu kuishawishi Iran iachane na urutubishaji wa madini ya uranium, shughuli inayoweza kutumiwa kutengeneza silaha za nyuklia.

Hata hivyo Sergei Lavrov amependekeza kuwa ripoti ya Marekani huenda ikalikwamisha azimio la tatu la vikwazo dhidi ya Iran ambalo Marekani inalishinikiza katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Wakati haya yakiarifiwa kiongozi wa shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za nyuklia, Mohammed El Baradei, amesema leo kwamba ripoti ya Marekani inaipa nafasi Iran kuutanzua mzozo wake wa nyuklia. El Baradei ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Brasilia nchini Brazil.

Naye waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni leo ameonya mjini Jerusalem, dhidi ya kulegeza msimamo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuwataka viongozi duniani waunge mkono vikwazo vipya dhidi ya utawala wa rais Mahmoud Ahmadinejad.